Jezi ya Simba yaipiga bao ya Yanga

JEZI za Simba ndizo zimeonekana kuwa nyingi eneo la Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa huku zile za watani wao Yanga zikiwa za kuhesabika.
Leo Jumatatu Agosti 31, 2020 Simba inacheza mechi ya kirafiki na AFC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo nje ya uwanja kuna wafanyabiashara wanauza jezi hizo lakini jezi za Simba pekee ndizo zimetandazwa kwa wingi.
Mmoja wa wafanyabiashara hao Emmanuel Mgonja amesema kuwa mauzo ya jezi za Yanga msimu huu yamekuwa hafifu ndio sababu kubwa ya kushindwa kuendelea kununua jezi hizo.
Amesema kuwa udhibiti wa jezi za Yanga uliofanywa na kampuni inayowadhamini GSM pia imefanya jezi hizo kuadimika viwanjani.
"Huwa nasafiri mikoani kuuza tu jezi pale michezo ya timu hizi zinapocheza lakini tangu kuanza kwa msimu ulioisha jezi hizo zimekuwa hazilipi, kwani zinatoka moja moja sana, pia GSM wamekuwa wakifanya ukaguzi mno juu ya hizo jezi na ukikamatwa nazo bila kibali ni kesi," amesema Mgonja
Amina Mohamed amesema mauzo ya jezi za Yanga ni madogo kutokana na timu hiyo kutokufanya vizuri msimu uliopita ikiwemo kukosa makombe ya michuano yote.