Prime
Huyu hapa kocha mpya Simba

Muktasari:
- Simba wanaamini kwamba anaweza kurithi mikoba iliyoachwa na Mualgeria Abdelhack Benchikha kwani safari hii wanasaka bosi ambaye hana wasifu mkubwa lakini ana uchu wa mafanikio.
MWANASPOTI linajua Simba iko kwenye mazungumzo na kocha Msauzi,Steve Komphela (56) na yamefikia katika hatua nzuri kama ilivyo kwa Mido wa Asec,Serge Pokou. Ni chuma kwa chuma mpaka Simba mpya ikamilike.
Simba wanaamini kwamba anaweza kurithi mikoba iliyoachwa na Mualgeria Abdelhack Benchikha kwani safari hii wanasaka bosi ambaye hana wasifu mkubwa lakini ana uchu wa mafanikio.
Viongozi wa Simba wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Salim Abdallah ‘Try Again’ kwa nyakati tofauti wamekuwa wakifanya vikao na Kompela kupitia mtandao wa ‘Zoom’ kwa lengo la kumpa mkataba kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs.
“Ni kocha mzuri ambaye naamini anaweza kuendana na falsafa yetu ukizingatia kwa sasa tunasuka timu mpya itakayotupa heshima katika msimu ijayo,” alisema kiongozi huyo na kumsifia Komphela kama miongoni mwa vichwa vinavyokuja kwa kasi kwenye soka la Afrika.
Katika msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Afrika Kusini alikuwa na kikosi cha Golden Arrow alichojiunga nacho Machi mwaka huu na kumaliza nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi hiyo lakini kabla ya hapo alikuwa kocha mkuu wa Moloka Swallows iliyomaliza katika nafasi ya 14 kwenye ligi hiyo.
Kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 alikuwa msaidizi wa Kocha Rulan Mokwena katika kikosi cha Mamelodi Sundowns lakini kabla ya hapo alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo kwa kuanzia mwaka 2020 hadi 2022.
Ukiachana na timu hizo, Mwaka 2015 hadi 2018 alikuwa kocha mkuu wa Kaizer Chiefs lakini pia kabla ya hapo aliinoa Maritzburg United kuanzia 2014 hadi 2015.
Sio kocha wa viwango vidogo kwani mwaka 2012 aliwahi kukaimu nafasi ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Afrika kusini lakini huko nyuma aliwahi kuzifundisha FS Stars, Platinum Stars, Dynamos FC, Manning Rangers na timu ya vijana (U-20), ya Afrika Kusini.
Ukiachana na ukocha pia Komphela aliwahi kucheza soka kwa mafanikio katika klabu za Qwa Qwa Stars na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini sambamba na Gazianterpspor, C. Dardanelspor naDardanelspor za Uturuki bila kusahau timu ya taifa ya Afrika Kusini.