Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huyo Bwalya mtu hatari

SIMBA imefuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kibabe baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 nyumbani juzi dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, lakini nyuma ya matokeo hayo huwezi kuliacha jina la kiungo, Larry Bwalya na soka la nguvu la Joash Onyango.

Kiungo huyo Mzambia alikuwa mwiba kwa Platinum kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa Simba juzi katika eneo la katikati mwa uwanja jambo lililowadhohofisha wapinzani wao na kuipa uimara mkubwa timu yake, huku Onyango naye akisafisha kila uchafu langoni mwake.

Bwalya ambaye kwa muda mrefu hakuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba, alitawanya vyema mipira na kuichezesha timu, kushiriki katika kutibua mipango ya viungo wa timu pinzani na kuisukuma timu mbele jambo lililoifanya Simba kuwa tishio katika muda mwingi wa mechi hiyo.

Ni mechi ambayo kwa kiasi kikubwa ilitawaliwa na Simba ambao mbali ya kumiliki mpira, walitengeneza nafasi nyingi ambazo kama wangezitumia vizuri wangeweza kuibuka na ushindi mnono zaidi ya huo wa mabao 4-0.

Kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza, Platinum iliingia na mbinu ya kujilinda ikijaza idadi kubwa ya wachezaji katika eneo lao la ulinzi na kujaribu kushambulia kwa kushtukiza kwa kupiga mipira mirefu kwenda kwa Perfect Chikwende na Denzel Khumalo ambao hata hivyo hawakufua dafu mbele ya mabeki wa Simba wakiongozwa na Onyango aliyekuwa katika ubora.

Chikwende aliyeonekana tishio katika mechi ya kwanza ambayo ndio alifunga bao pekee la ushindi kwa Platinum, juzi alijikuta akiwa katika wakati mgumu mbele ya ukuta wa Simba ambao ulimudu kuidhibiti mikimbio yake na kutompa nafasi ya kulisogelea lango lao.

Utulivu na umakini wa nyota wa Simba, uliwasaidia kwa kiasi kikubwa wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuibuka na ushindi huo muhimu mbele ya Platinum ambao mara kwa mara walionekana kupaniki na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.

Kama isingekuwa busara ya mwamuzi Georges Gatogato kutoka Burundi, kundi kubwa la wachezaji wa Platinum wangeweza kuonyeshwa kadi kwani mara kwa mara walikuwa wakimzonga na kumfokea wakionyesha kutokukubaliana na maamuzi yake hasa penalti iliyowatanguliza Simba kwenye mchezo huo ikifungwa na Erasto Nyoni.

Mwanaspoti lilikuwa uwanjani na limefanya tathmini ya mchango wa kila mchezaji kwa timu yake katika mechi hiyo.