Simba macho katika makundi

Muktasari:
Simba imetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1 wa mechi mbili.
Dar es Salaam. Wakati droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikipangwa kuchezeshwa leo, wawakilishi wa Tanzania katika hatua hiyo, Simba huenda wakapangwa katika kundi lenye timu tishio kutoka kaskazini mwa Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), droo hiyo itafanyika leo saa 9.00 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki katika makao makuu ya shirikisho hilo yaliyopo mjini Cairo, Misri.
“Washindi wa jumla wa hatua ya kwanza ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watahusika katika droo ya makundi na washindi wa jumla wa hatua ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika watashiriki katika droo ya mwisho ya mchujo,” ilisema taarifa hiyo ya Caf.

Kutokana na utaratibu wa uchezeshaji droo hiyo ulioainishwa na Caf, upo uwezekano wa Simba kupangwa katika kundi lenye timu vigogo hasa zile za kutoka Kaskazini mwa Afrika, ambazo zimekuwa na uzoefu mkubwa na rekodi ya kufanya vizuri katika mashindano hayo, lakini pia zimekuwa na uwekezaji mkubwa wa fedha, ambao umeziwezesha kusajili wachezaji bora na wa daraja la juu, ambao wanalipwa fedha nyingi na kuhudumiwa vizuri.
Kutokana na pointi zake ilizokusanya katika viwango vya timu zilizofanya vizuri kimataifa, katika droo hiyo, Simba imepangwa katika chungu cha tatu ambacho kitakuwa pia na timu za Al Hilal/Asante Kotoko, Pero de Luanda ya Angola pamoja na MC Alger ya Algeria.
Kwa kuweka katika chungu cha tatu, inamaanisha kwamba Simba haitoweza kukutana na timu nyingine tatu za chungu hicho bali itapangwa katika kundi ambalo litajumuisha pia timu kutoka chungu cha kwanza, cha pili na cha nne.

Vigogo 11 ambavyo Simba inaweza kuangukia katika kundi moja na tatu miongoni mwa hivyo ni Wydad Casablanca (Morocco), Esperance (Tunisia), Al Ahly na Zamalek (Misri), TP Mazembe na AS Vita (DR Congo), Mamelodi Sundowns na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini), Horoya (Guinea) pamoja na CR Belouizdad ya Algeria.
Mazembe, Al Ahly, Wydad na Esperance zenyewe zipo chungu cha kwanza na kila moja itapewa uongozi wa kundi, na zilizopo chungu cha pili ni Mamelodi, AS Vita, Zamalek na Horoya.
Chungu cha nne kitakuwa na Belouizdad, Al Merrikh (Sudan), Kaizer Chiefs na Teungueth (Senegal).
Al Ahly ni mabingwa wa kihistoria wa taji hilo wakiwa wamelitwaa mara tisa, wakati Mazembe na Zamalek kila moja imekuwa bingwa mara tano tofauti wa mashindano hayo.
Timu nyingine na idadi ya mataji ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizochukua ni Esperance mara nne, Wydad Casablanca (2), AS Vita (1) na Mamelodi imechukua mara moja.