Huo Mchongo wa Mwanaspoti usipime!

Muktasari:
- Mkuu wa Maudhui wa MCL, Frank Sanga alisema kwa sasa wasomaji wa michezo nchini wanapata habari motomoto na zilizofanyiwa utafiti wa kina.
UNAACHAJE sasa mchongo huu wa kijanja? Ndio. Promosheni ya Shinda Mchongo ya Mwanaspoti imezinduliwa rasmi jana Jumatatu ikitoa fursa kwa wasomaji wa gazeti hili kujizolea zawadi kedekede kwa muda wa wiki 12.
Promosheni hiyo imezinduliwa makao makuu ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na Mkurugenzi Mtendaji, Francis Nanai, huku ikishuhudiwa na mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha, Jehud Ngolo.
Nanai alisema lengo la promosheni hiyo ni kuwashukuru wasomaji kwa kuendelea kulichagua Mwanaspoti kuwa suluhisho la mahitaji yao kwa habari za michezo na burudani nchini.
Alisema tangu mwaka 2001 lilipoanzishwa, Mwanaspoti limekuwa gazeti bora kwa habari za michezo na burudani nchini na kwamba, Promosheni ya Mchongo wa Mwanaspoti inakwenda sambamba na uboreshwaji wa maudhui.
“Kupitia gazeti la Mwanaspoti wateja wetu watapata zawadi mbalimbali katika promosheni hii, ambapo kila wiki watakuwa wanapatikana washindi watano watakaojishindia zawadi ya Sh100,000 taslimu,” alisema.
“Tunawapenda wasomaji wetu na siku zote tumekuwa karibu kuhakikisha wanafurahia huduma tunayowapa. Kama mtaangalia mtaona kuanzia Juni Mosi tumeboresha maudhui, muonekano na kuongeza kurasa ili kukata kiu ya wasomaji.”
Mkuu wa Maudhui wa MCL, Frank Sanga alisema kwa sasa wasomaji wa michezo nchini wanapata habari motomoto na zilizofanyiwa utafiti wa kina.
Alisema kuna mabadiliko makubwa yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuongeza kurasa na muonekano mpya huku majarida mapya ya Ze Kick na Wikiend Vibe yakiongezwa kunogesha ladha.
“Mwanaspoti ndilo gazeti bora la michezo kwa ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo mbali na Tanzania pia linapatikana kule Kenya na kuanzia Juni Mosi, limekuja kivingine kabisa likikupa habari motomoto zinazokidhi mahitaji ya wasomaji,” alisema Sanga.
Meneja wa Masoko wa MCL, Sarah Munema alisema mbali na zawadi za pesa taslimu na bodaboda, pia kutakuwa na zawadi kubwa ya Sh10 milioni kwenye droo ya mwisho.
Alisema washindi wa mwisho wa droo kubwa watajishindia kitita cha Sh5 milioni kila mmoja na droo ya kwanza itakuwa Julai 14, mwaka huu, ambapo itarushwa na kituo cha luninga cha Azam.
“Unachotakiwa kufanya ni kununua gazeti la Mwanaspoti na ukurasa wa pili utakuta kuponi ijaze ukiweka taarifa zako sahihi kisha tuma ofisini kwetu ama kabidhi kwa wauza magazeti waliopo jirani nayo. Cheza mara nyingi ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi ya kushinda,” alisema Sarah.
Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Ngolo aliwatoa hofu wasomaji na washiriki wa promosheni hiyo kuwa, kila kitu kitakwenda sawa kwa vile si mara ya kwanza kwa Mwaaspoti kuendesha promosheni kama hiyo.