Homeboys, Tusker hapatoshi

Wednesday April 27 2022
Tusker PIC
By Isiji Dominic
By Sinda Matiko

MABINGWA watetezi Ligi Kuu Kenya, Tusker FC, wanazidi kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wao huku presha ikionekana kupanda kwa Kakamega Homeboyz ambao kwa muda mrefu wamekuwa kileleni.

Tusker FC walianza wikendi iliyopita wakiwa pointi nane nyuma ya vinara Kakamega Homeboyz lakini wamemaliza wikendi kwa tofauti ya pointi sita hivyo kunogesha mbio za ubingwa FKFPL msimu huu.

Vijana wa Robert ‘Simba’ Matano walihitaji bao dakika za mwisho lililofungwa na Deogratius Ojok kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AFC Leopards katika mchezo mkali na wa kusisimua kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi.

Awali Tusker FC walitangulia kupata bao iliyofungwa na Lawrence Luvanda kipindi cha kwanza lakini zikiwa zimesalia dakika nane mpira kumalizika, Fasanami Olaniyi, aliisawazishia Ingwe hata hivyo haikutosha kuondoka na pointi moja. Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa Tusker FC na umekuja wiki moja tu baada ya kuwafunga Gor Mahia mabao 2-0 na Matano aliwamiminia sifa Ingwe kwa kuonyesha kandanda safi.

Utata katika mechi hiyo ilikua bao la Ojok na makocha Matano na Patrick Aussems wa Leopards walitofautiana.

“Nimeona picha za marudio, kulikuwa na mchezaji wa AFC Leopards aliyemfanya Ojok asiwe kwenye eneo la kuotea na sijui kwa nini wanadai lilikua bao la kuotea,” alisema Matano.

Advertisement

Hata hivyo, Aussems aliyeshuhudia timu yake ikipoteza kwa mara ya kwanza baada ya mechi 11, alisisitiza Ojok alikuwa ameotea.

Wakati Tusker FC wakishinda mechi mbili kwa mpigo, Homeboyz walilazimishwa sare ya tatu mfululizo na Kenya Police FC mechi ikimalizika kwa mabao 2-2.

Ni sare ambayo haikumfurahsha kocha msaidizi wa Homeboyz, Eric Muranda, lakini akaahidi kurekebisha makosa ili timu irudi katika kushinda mechi zake.

“Ligi ni marathon na hadi hapo iwe imeshindikana kimahesabu, hatuwezi kuhitimisha kuwa kuna wale wanaopewa nafasi kubwa kutwaa ubingwa au kushuka daraja,” alisema.

Licha ya Homeboyz kudondosha alama tena, Kocha mkuu, Bernard Mwalala kazidi kujishasha haitakuwa rahisi wao kubanduliwa kileleni.

Mwalala aliyeamua kuwahepa wanahabari baada ya mchezo wao huo, juzi Jumapili uwanja wa Kasarani Annex, bado kachocha kuibandiua timu yake kileleni, haitakuwa rahisi. “Bwana ligi ni sawa na marathon hivyo hatuwezi kutumia matokeo ya mechi moja kama kigezo cha kuhoji ikiwa tuna uwezo au la wa kushinda kombe la ligi kuu msimu huu. Nasisitiza tena sidhani matokeo yetu ya juzi yana athari zozote kwenye mchakato wetu wa kusaka taji la ligi kuu msimu huu. Ndio tumedondosha alama lakini usisahahu hata nayo alama moja hiyo tuliyopata ni muhimu sana kwenye harakati zetu za kushinda ligi,” Mwalala kajichocha. Zikiwa sasa zimesalia mechi saba tu za msimu huu huku timu zote kwenye top 3 zikiwa zimecheza jumla ya mechi 27 kila moja, Homeboyz wangali wamedatia keleleni.

“Tunakaribia utepeni na alama moja hiyo imetubeba. Imetuwezesha kupiga hatua nyingine kuelekea kwenye ushindi wa kombe,” Mwalala kasisitiza.

Hofu ya Homeboyz mbio za ubingwa wa ligi, haipo tu kwa Tusker FC mbali pia kwa Nairobi City Stars na Gor Mahia kila moja akijikusanyia pointi 45 japo walikuwa na matokeo tofauti mwishoni mwa wiki iliyopita.

K’Ogalo wao waliwafunga KCB bao 1-0 lakini Nairobi City Stars wakicheza pungufu baada ya Anthony Kimani Njoroge kutolewa nje kwa kadi nyekundu walikubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Sofapaka.

Huku ushindani ukionekana kuwa mkali kwa timu zinazowania ubingwa, hali imekuwa ndivyo sivyo kwa Mathare United wakishindwa kupeleka timu uwanjani kuikabili Bandari FC kutokana na ukata.

Matokeo yake, Bandari FC walipata ushindi wa mezani na macho sasa yapo kwa kamati shikilizi ya Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuona ni maamuzi yapi watakayochukua dhidi ya Mathare United ambayo haijawahi kususia mechi tangu ianze kushiriki ligi miaka 28 iliyopita.


Advertisement