Hitimana apika Luis, Chama wapya

SIKU chache baada ya kutua Simba, kocha msaidizi wa timu hiyo, Hitimana Thiery amesema licha ya ubora wa nyota wao, kwa sasa wanapambana kutengeneza pacha mpya ili kuziba pengo la Clatous Chama na Luis Miquissone.

Chama na Luis walikuwa na msimu mzuri ndani ya Simba wakihusika katika mabao 41 baada ya Chama kufunga mabao 8 na kutoa asisti 13, huku Luis alifunga mabao 9 na kutoa asisti 11, idadi ambayo ni zaidi ya nusu ya mabao 74 yaliyofungwa na Simba nzima katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Luis aliuzwa kwa Al Ahly ya nchini Misri, huku Chama akitua Berkane FC ya Morocco na sasa benchi la ufundi linaumiza vichwa kuyarudisha mabao hayo 41.

Simba inatarajia kuwatumia wachezaji kama Ousmane Sakho, Yusuph Mhilu, Duncan Nyoni, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga na Peter Banda ambao wanaweza kuwa mbadala wa Chama na Miquisone.

Akizungumza na Mwanaspoti, Hitimana alisema tangu aingie kikosini humo, amefurahishwa na ubora wa nyota waliopo lakini ishu kubwa ipo kwenye kuzipa mapengo ya wachezaji walioondoka.

Alisema iwapo mipango yao itatiki hasa kupata mbadala wa Chama na Luis na matokeo mazuri mambo yanaweza kuwanyookea vinginevyo kutakuwa na ugumu.

“Wachezaji ni wazuri na kila mmoja anaonyesha uwezo wake na kama tutaweza kuziba mapengo ya Chama na Luis itakuwa vizuri zaidi,” alisema huku akieleza kufurahishwa na upambanaji wa nyota wote kikosini mwake.