Haya sasa kumekucha, Wakongo kuunda ukuta mpya Yanga

KOCHA wa Yanga, Nesreddine Nabi amewawekea viongozi majina mawili ya mabeki wa kati akawasisitiza kwamba ; “Nataka mmoja hapo.”

Walivyofungua wakati yeye akiwa amewasimamia ameshika kiuno wakakuta ni Marcel Kalonda na Hennock Inonga Baka. Wote ni raia wa DR Congo ambao kwenye mitandao ya kijamii rekodi zao zinaonyesha ni wachezaji ambao bei zao si za kitoto kwavile bado wako imara kiushindani na wanauzika kwa gharama kubwa.

Tayari Mwanaspoti linajua kwamba Yanga imeshamalizana na Djuma Shabaan ambaye ni beki Mkongomani, Dickson Ambundo wa Dodoma Jiji ambaye ni winga na beki wa kushoto David Brayson wa KMC.

Majina hayo mawili mapya mpaka jana yalikuwa yanawaumiza vichwa Yanga na tayari wameshaanza mazungumzo na kila mmoja na kabla ya wikiendi hii watakuwa wamemalizana na yoyote kati yao.

Mwanaspoti linajua kwamba Yanga inatafuta beki wa kati wa haraka ambaye ni mtu wa kazi na ni agizo la Nabi ambaye anataka pia timu mpya irudi kambini mapema.


Marcel Kalonda

Amemaliza msimu wa nne na Zesco ya Zambia ambao ni mabingwa wa nchi hiyo.

Kalonda anajulikana kwa shughuli moja tu kupambana na washambuliaji wakorofi na kiungo wa Yanga wa zamani Thabani Kamusoko ameliambia Mwanaspoti kwamba jamaa anajua kama wakimpata ni usajili mzuri.

“Nimemkuta hapa Zesco ni beki wa kazi hasa anajua kukaba lakini pia ni mzuri katika mipira ya juu sijajua kama Zesco watamuachia kwani ndio beki wao wa muhimu,”alisema Kamusoko ambaye aliwahi kufanya kazi ya maana Yanga kisha akatimkia Zesco.


HENNOCK

Huyu anakipiga sana timu ya Taifa ya DR Congo akiitumikia DC Motema Pembe. Inonga aliwahi kutajwa pia Simba lakini wakashindwa kukubaliana mkwanja, ni mtu na nusu kwani wachambuzi wa Congo wanasema sio rahisi kufunga mbele yake.

Inonga Mwanaspoti linafahamu kwamba jina lake lilipenyezwa na kocha wa zamani wa AS Vita,Florent Ibenge wakati alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Yanga Injinia Hersi Said hivi karibuni jijini Casablanca nchini Morocco.

Ibenge anamuamini Ilonga na ndio kocha wa kwanza kumuita timu ya taifa ya nchi hilo ambapo tangu aitwe amekuwa hakosekani kwa makocha wengine.

Yanga inapiga hesabu za kuchukua mmoja kati ya hawa Wakongomani wawili ili wazibe nafasi ya nahodha wao Mkuu Lamine Moro ambaye hawaivi na Nabi kutokana na mwenendo wake wa hivikaribuni na muda wowote ataaga Tanzania kama mmoja wa hao atapatikana.

Nabi amewaambia mabosi wa Yanga kabla ya kuachana na Moro watafute kwanza beki wa maana atakayekuwa na kimo kizuri lakini pia awe na ubora wa kuanzisha mashambulizi na kukabiliana na mipira ya juu sifa ambazo ni kitu cha kawaida kwa Wakongomani hao.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba wanapambana na mahitaji ya mabeki hao katika gharama za usajili ili wafanye uamuzi wa yupi wanamchukua na hilo litafanyika kwa haraka sana. Juzi na Jana Yanga walikuwa na kikao kizito cha kufanya uamuzi wa mwisho.

Mwanaspoti linajua kwamba kesho Senzo Mazingisa na Hersi Said watakwea ndege tofauti kwenda kumalizana na silaha zisizopungua nane za Yanga wakiwemo Wakongomani hao.


KAGAME WAMO

Mmoja wa viongozi wa Yanga alisema kuwa;”Tutashiriki mashindano haya na wachezaji ambao walikuwa hawapati muda mwingi wa kucheza, wengine wanaoweza kushiriki ni hawa wapya wote ili wapate muda wa kucheza pia kabla hatujaanza maandalizi ya msimu mpya.”

“Tutatoa programu zetu zote na zitakuwa wazi namna tutakavyojiandaa na msimu mpya,” alisema kigogo huyo.

Mashindano ya Kagame yanafanyika Agosti mosi mpaka 15 mwaka huu, huku Yanga wao wakitazamia kuweka kambi baada ya wiki mbili mwezi ujao nchini Morocco.