Hawa wana balaa katika kupiga faulo, si utani

Ramadhan Singano "Messi"
Muktasari:
Mwanaspoti imekuchambualia wakali wa mipira ya faulo wa klabu zote 14 za ligi na mambo ambayo wamefanya kwenye mechi saba za kwanza za mzunguko wa kwanza uliosimama;
KUPIGA faulo ni zoezi gumu na vilevile ni kipaji. Katika Ligi Kuu Bara kuna wachezaji wachache wa aina hiyo ambao wanapopiga mipira ya michache ya namna hiyo wakikukosa ujue una bahati.
Mwanaspoti imekuchambualia wakali wa mipira ya faulo wa klabu zote 14 za ligi na mambo ambayo wamefanya kwenye mechi saba za kwanza za mzunguko wa kwanza uliosimama;
Ramadhani Salim ‘Rama’ (Coastal Union)
Kabla ya kuwataja wakali wote wa mipira ya faulo, jina la Mkenya, Rama Salim ni lazima uliweke namba moja. Rama ambaye tayari ameshafunga mabao mawili kwa njia hiyo ya faulo, amekuwa tishio kutokana na uhodari wake huo.
Hana mwili mkubwa lakini ana makadirio mazuri ya hesabu kutoka mahali anapopiga mpira na goli la wapinzani. Alifunga bao la kwanza la faulo kwa ustadi walipotoa sare ya 2-2 na Simba Uwanja wa Taifa na bao lake la pili la aina hiyo, walipofungwa na Azam FC bao 2-1. Ameanza kuichezea Coastal msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya.
Andrey Coutinho (Yanga)
Huyu ni kiungo Mbrazili ambaye ni mzuri zaidi anapocheza winga ya kushoto, amepata umaarufu kwenye kikosi cha Yanga pamoja na soka la Tanzania kutokana na ubora wake wa kupiga faulo zenye kuzaa mabao.
Alithibitisha ubora wake huo baada ya kupachika bao la namna hiyo kwenye mechi yao na Prisons walipotoka na ushindi wa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Coutinho anayetumia mguu wa kushoto zaidi, amekuwa hatari katika kupiga faulo zinazotokea upande wao wa kulia.
Haruna Niyonzima (Yanga)
Niyonzima ni Mnyarwanda ambaye ni kiungo mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumia miguu yote, ana nguvu lakini hana umbo la kutisha.
Ndiyo tegemeo la Yanga katika upigaji wa faulo na ameweka historia baada ya kupachika bao la namna hiyo katika mechi waliyoifunga JKT Ruvu mabao 2-1.
Faulo hiyo ilipigwa kiustadi na kwenda moja kwa moja golini na kuwaacha midomo wazi wachezaji wa JKT ambao waliweka ukuta kuzuia pamoja na kipa wao, Jackson Chove.
Mbuyu Twite (Yanga)
Huyu ni Mnyarwanda mwenye asili ya Congo ni hodari wa kupiga mipira ya faulo ya mbali kama mita 25 au zaidi na kuwa bao. Mwenyewe amekiri upigaji wa penalti unamsumbua lakini kwenye faulo za mbali yuko mbali.
Emmanuel Okwi (Simba)
Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi raia wa Uganda tayari ametengeneza rekodi yake baada ya kufunga bao la faulo katika mechi yao waliyotoa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Okwi ambaye anatambulika kuwa na chenga za maudhi ameonyesha ustadi huo wa kupiga faulo zilizo karibu na eneo la 18.
Shaaban Kisiga (Simba)
Kiungo wa Simba, Shaaban Kisiga mkongwe ambaye alirudi kikosini hapo kwa mara nyingine akitokea Mtibwa Sugar ni hatari mno kwenye mipira ya faulo.
Faulo hizo, zimemjengea heshima kikosini hapo baada ya kuifungia timu hiyo, bao pekee lililowapa sare ya 1-1 dhidi ya Stendi. Anajua kupiga faulo za karibu nje kidogo ya 18 na za mbali pia.
Ramadhani Singano ‘Messi’ (Simba)
Mshambuliaji, Ramadhani Singano ‘Messi’ ni chaguo lingine la Simba katika upigaji wa faulo za mbali.
Msimu huu hajapata nafasi sana kwa sababu ya uwepo wa Kisiga na Okwi.
Kipre Bolou, Erasto Nyoni na Mcha (Azam FC)
Kiungo Muivory Coast wa Azam FC, Kipre Bolou, kiraka Erasto Nyoni na mshambuliaji Mcha Hamis ndiyo wanaotesa kwenye kikosi cha Azam kwa upigaji mzuri wa mipira ya faulo lakini hata ile ya penalti.
Wote wana uwezo wa kupiga faulo za mbali lakini Mcha na Nyoni pia wanaweza kupiga zilizokaribu na eneo la 18.
Najim Magulu, Jabir Aziz na Faki (JKT Ruvu)
Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Felix Minziro amekuwa akiwatumia wachezaji, Najim Magulu, Jabir Aziz na Mohamed Faki katika upigaji wa faulo.
Wote wanaweza kupiga mapigo ya mbali ingawa Najim ni mzuri zaidi kwa mipira iliyo karibu na eneo la 18.
Salum Kanoni (Kagera Sugar)
Sifa kuu wa beki wa kulia wa Kagera Sugar, Salum Kanoni ni upigaji wa mipira ya adhabu hasa faulo. Kagera inamtumia, Kanoni ambaye aliwahi kuichezea Simba miaka ya nyuma katika faulo zote zilizo karibu na eneo la 18 na umbali mkubwa.
David Luhende na Hassan Kessy (Mtibwa)
Mtibwa ambayo ndiyo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kujikusanyia pointi 15 na Azam na Yanga zinamfuata kwa pointi 13.
Imekuwa ikiwatumia mabeki, David Luhende na Hassan Kessy katika upigaji wa faulo zote za mbali na karibu ya eneo la 18. Wachezaji hao pia ni hodari kwenye upigaji wa penalti.
Busungu Malimi (Mgambo)
Ni mshambuliaji wa Mgambo Shooting, Busungu Malimi ambaye msimu ujao huenda akatua kuichezea Yanga. Ndiye tegemeo wa Mgambo katika upigaji wa faulo kwa mapigo ya mbali na karibu.
Yusuph Nguya, Michael Idani na Lambele
(Ruvu Shooting)
Inapotokea mipira yote ya faulo kwa klabu ya Ruvu Shooting iliyo karibu na eneo la 18, straika Jerome Lambele ndiyo anahusika. Lakini inapokuwa kwenye umbali mkubwa, mabeki Yusuph Nguya na Michael Idani ndiyo wanapiga.
Iddi Kulachi (Ndanda FC)
Kocha Mkuu wa Ndanda FC, Meja mstaafu, Abdul Mingange amempa majukumu ya kupiga faulo zote, Iddi Kulachi. Kulachi ameonyesha ustadi wa kupiga faulo zote za mbali na karibu na tayari ameshafunga bao moja la namna hiyo.
Bao hilo la faulo alilifunga katika mechi waliyofungwa na Mtibwa 3-1 wakafutia machozi.
Danny Mrwanda, Nahoda Bakari (Polisi Morogoro)
Maafande wa Polisi Morogoro, wanawategemea zaidi, Danny Mrwanda na
Nahoda Bakari katika upigaji wa mipira yote ya faulo inayotokea.
Salum Machaku alikuwa miongoni mwao, lakini yeye hakuwa na timu kwa takribani mechi nne za mwishoni kwa kile kinachodaiwa ana matatizo ya kifamilia.
Mrwanda anayewaniwa na Simba ni mkali pia kwenye penalti na kati ya mabao yake manne moja amefungwa kwa njia ya penalti.
Ray Mgungira, Mussa Mussa, Iddi Mobi (Stand United)
Stand United iliyopanda Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza imekuwa ikiwatumia Ray Mgungira, Mussa Mussa, Iddi Mobi kunapotokea faulo zote za mbali.Ingawa, Mgungira na Mobi ni wazuri pia kwenye faulo zilizo karibu na eneo la 18.
Jeremia Juma na Ibrahim Mamba (Tanzania Prisons)
Maafande wa Tanzania Prisons chini ya kocha, David Mwamaja imekuwa ikiwatumia wachezaji tofauti ambao wanakuwa vizuri kulingana na mchezo husika.
Lakini, Jeremia Juma na Ibrahim Mamba ndiyo tegemeo lao katika upigaji wa faulo.
Hamad Kibopile, Steven Mazanda (Mbeya City)
Klabu ya Mbeya City ambayo sasa inashika mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, imekuwa ikiwategemea zaidi, Steven Mazanda na Hamad Kibopile katika upigaji wa faulo.