Hawa jamaa noma, wanakomaa na ndondo mwanzo mwisho

Muktasari:
Lakini ikumbukwe kwamba mtaani kuna wachezaji wengi ambao hawashiriki mashindano makubwa kama Ligi Kuu au hata zile ligi ndogo zilizo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), hivyo huamua kubuni mashindano mengine ya makombe ambayo hushirikisha timu za mtaani kama kombe la jezi, ng’ombe, mbuzi na mengineyo.
WACHEZAJI wengi wa Ligi Kuu Bara wanapokuwa katika kipindi cha mapumziko baadhi yao hutumia mapumziko hayo kwa kufanya mazoezi binafsi ambayo ni mepesi ili kujiweka fiti kwa matukio yaliyo mbele yao.
Lakini ikumbukwe kwamba mtaani kuna wachezaji wengi ambao hawashiriki mashindano makubwa kama Ligi Kuu au hata zile ligi ndogo zilizo chini ya Shirikisho la Soka nchini (TFF), hivyo huamua kubuni mashindano mengine ya makombe ambayo hushirikisha timu za mtaani kama kombe la jezi, ng’ombe, mbuzi na mengineyo.
Mechi hizo mara nyingi hujulikana kama ndondo ambazo baadhi ya wachezaji wa ligi hushiriki ikiwa ni njia ya kufanya mazoezi na kujiweka fiti wakisubiri kurudi kwenye ligi ingawa baadhi ya timu huwa haziruhusu wachezaji wao kushiriki mechi hizo wakihofia kuumia kwani gharama za kuwatibu zinakuwa juu ya waajiri wa wachezaji hao.
Baadhi ya timu ambazo hukataza wachezaji wake wasicheze ndondo ni Simba, Azam na Yanga ambazo zilitangaza wazi kwamba mchezaji wao akibainika amecheza mechi za ndondo basi atakatwa Sh 400,000 kutoka kwenye mshahara wake wa mwezi.
Baadhi ya maeneo maarufu ambayo mara nyingi unaweza kuwakuta wachezaji hao ni maeneo ya Tabata Shule, Sinza-Kinesi, Tandika-Bandari, Yombo, Magomeni -Makurumla, Mwananyamala B na Vingunguti. Uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kwamba wachezaji wa timu za Ligi Kuu hupenda kucheza mechi hizo kujipatia kipato cha ziada cha harakaharaka kwavile waandaaji wa mechi hizo hupenda wawepo ili kuongeza mashabiki na mvuto wa mashindano.
Ingawa wachezaji hutumia mechi hizo kama sehemu ya mazoezi, mara nyingi hulipwa kati ya Sh20,000, 50,000 na 100,000 kulingana na mfuko wa mwaandaaji na umaarufu wa mchezaji. Uchunguzi umebaini kwamba wachezaji wengi hufanya mechi hizo kama siri na hata wanapoumia hujikaza wanaporudi kwenye klabu zao ili isibainike kwamba waumia mchangani. Marafiki wa karibu wa baadhi ya wachezaji hao wanadai kwamba hata wachezaji wanavyosemwa kwenye klabu zao kwamba wanachezaji chini ya kiwango ni kutokana na maumivu ambayo huyapata kwenye viwanja chakavu vya mchangani na kujikaza kwa kuhofia kufukuzwa katika klabu zao.
Ingawa Dar es Salaam kuna wachezaji wengi ambao hucheza mechi hizo, hawa ni baadhi ya wachezaji ambao huonekana waziwazi wakicheza mara kwa mara ingawa wamekuwa wakisisitiza kwamba ni katika kujiweka fiti tu, kulinda hadhi ya timu zao za mchangani ambazo ndizo zimewakuza kisoka tangu wakiwa wadogo wala si kutafuta fedha.
Jerry Tegete -Yanga
Hivi karibuni mshambuliaji wa Yanga, Jerryson Tegete, alikaririwa akiwaomba viongozi wake kuwaruhusu kucheza mechi za ndondo wanapokuwa kwenye mapumziko kwa maelezo kwamba wanachukuwa muda mrefu kukaa nje ya uwanja bila kucheza wakisubiri mechi za ligi.
Katika michuano iliyomalizika wiki iliyopita ya fainali za Kombe la Ndondo, Tegete ndiye aliyeipatia timu yake ya Tabata bao la ushindi katika fainali hizo ambazo Abajalo ilitwaa ubingwa huo kwa mikwaju ya penalti. Inawezekana Yanga walisikia kilio cha mchezaji huyo na kumruhusu kucheza. Tegete amekuwa akifanya vizuri anacheza mechi hizo ambazo hata hivyo wachezaji wake wengi hawako fiti kwa vile hucheza tu ilimradi.
David Luhende - Mtibwa Sugar
Beki wa zamani wa Yanga, ambaye kwa sasa anaichezea Mtibwa Sugar naye ni miongoni mwa wachezaji wanaopenda kutumia likizo yao katika mechi za ndondo, hata kama kuna timu nyingine anaichezea huko mtaani lakini Luhende hupendelea zaidi kuichezea timu ya Tabata.
Si mara moja au mara mbili kwa beki huyo ambaye ameonekana kung’aa alipotua Mtibwa msimu huu bali hiyo ni kawaida kwake anapokuwa mapumzikoni. Ni miongoni mwa wachezaji ambao ukiwakuta kwenye ubora wao kwenye ndondo huwezi kujua kwamba ni mchezaji wa Ligi Kuu.
Godfrey Taita-Yanga
Kwa sasa Taita hana timu baada ya kutemwa Yanga. Beki huyo kwake si jambo la ajabu na anapaswa kucheza mechi hizo kwa sababu hana timu, hiyo inamsaidia kujiweka fiti endapo atapata timu nyingine ya kuichezea katika mashindano ya Ligi kuu ama hata Ligi Daraja la Kwanza ambayo imeonekana kubeba mastaa wengi walioachwa na timu za Ligi kuu, Taita pia hupendelea kucheza timu ya Tabata.
Razak Khalfan-Coastal Union
Kiungo wa Coastal Union, Razak Khalfan ambaye kwa sasa ni kama anawashiwa taa nyekundu ya kuashiria kuondolewa kwenye timu hiyo yenye maskani yake jijini Tanga baada ya kuanza kumtafutia timu itakayomchukuwa kwa mkopo, Razak ni miongoni mwa wachezaji wanaong’aa katika kikosi cha Tabata, ambayo huichezea anapokuwa kwenye mapumziko yake. Ni kati ya wachezaji ambao wamecheza sana mchangani na kwao hawaoni kama ni kitu cha ajabu na huenda akaathirika au kujisikia amekosa kitu kikubwa sana asipopasha na wana kitaani.
Mussa Hassan ‘Mgosi’ - Mtibwa Sugar
Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Motema Pembe ya DR Congo ambaye kwa sasa anakipiga katika timu ya Mtibwa Sugar, ni mtaalamu wa ndondo hasa anapokuwa kwenye mapumziko yake ligi. Mgosi kwa sasa ana mabao mawili katika msimu huu wa ligi.
Hapa sasa ni patamu zaidi, Mgosi hupendelea kujichanganya na mastaa wenzake katika timu ya Muhimbili inayokusanya nyota kama Juma Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban’, Kipa Juma Kaseja (Yanga), Ivo Mapunda (Simba), Ibrahim Chove (JKT Ruvu), Shaban Kado (Coastal Union), Manyika Peter Jr (Simba), Said Mohamed (Mtibwa Sugar) na wengine kibao. Timu hiyo hufanyia mazoezi yake katika Uwanja wa Muhimbili na ina msimamizi wao maalumu ambaye huwatafutia mechi ili kujipima ufiti wao.
Stanley Nkomola - JKT Ruvu
Nkomola ni moja ya nguzo imara katika kikosi cha JKT Ruvu kilicho chini ya kocha Felix Minziro, anacheza kama beki na ana uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi timu yake inaposhambuliwa, lakini ni beki ambaye haachi kuitumia likizo yake katika kushiriki mechi za mchangani, hana timu maalumu kwani timu yoyote itakayohitaji huduma yake basi yeye hasiti kutoa huduma hiyo.
Kwake inamsaidia kulinda kiwango chake kikubwa ni kuwa makini katika kukwepa majeraha ambayo yanaweza kumgharimu atakaporejea katika kikosi chake kilichomwajiri.
Peter Mutabuzi - Stand United
Beki wa Stand United, ambayo inashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza Peter Mutabuzi, naye hawezi kuacha kucheza mechi hizo kutokana na mazoea yake tangu alipokuwa akijifunza kucheza soka mpaka sasa anapocheza akiwa kwenye mapumziko ya ligi. Mutabuzi alisajiliwa na Stand United akitokea Kagera Sugar.
Seleman Kibuta - Coastal Union
Kibuta amejiunga na Coastal Union msimu huu wa Ligi Kuu akitokea Kagera Sugar na kabla ya hapo alikuwa akiichezea Toto African ambayo alishuka nayo daraja msimu wa 2011/12. Mara nyingi Kibuta hucheza mechi za mchangani.
Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ - Simba
Ni beki wa Simba. Tshabalala alisajiliwa na Simba akitokea Kagera Sugar ambayo ilimchukuwa kutoka Friends Rangers yenye maskani yake Manzese-Kagera.
Awali alipenda mechi za mchangani kwani alikuwa akikutana na wachezaji wanaocheza timu kubwa za Ligi Kuu ambao walimpa uzoefu mkubwa mpaka hapo alipofikia.