Hatma ya Simba ipo kwa Simba wenyewe ikiamua

Muktasari:
- Kutokana na hali hiyo bado tunaamini Simba kama itaendeleza ule umwamba wake wa kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya AS Vita basi tiketi ya robo fainali itawahusu safari hii, kwani endapo itashinda, itafikisha alama tisa zitakazowapa moja ya nafasi ya kusonga mbele.
NI kweli kila shabiki wa soka hususani wale wa Msimbazi wamenyong’onyeshwa na kipigo cha tatu ambacho timu yao ya Simba imekipata katika mechi zao za Kundi D kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ilifumuliwa mabao 2-0 na JS Saoura ya Algeria na kufanya iwe imepoteza mechi zake zote tatu za ugenini kwa kufungwa jumla ya mabao 12 bila wenyewe kufunga hata bao moja, kwani awali ilifungwa 5-0 na AS Vita ya DR Congo kisha kulala tena kwa idadi kama hiyo kwa Al Ahly ya Misri.
Matokeo ya usiku wa juzi Jumamosi yameifanya Simba kuporomoka kutoka nafasi ya pili iliokuwapo nyuma ya Wamisri hadi mkiani ikisaliwa na alama zao sita, huku JS Saoura ikipanda kileleni ikiishusha Al Ahly iliyolala 1-0 mbele ya Vita kwa kufikisha pointi nane.
Vita na Al Ahly zote zikiwa na alama saba ila zinatofautiana uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Kwa hesabu zilivyo, katika kundi hilo ni kwamba timu zote nne zina nafasi sawa ya kusonga mbele endapo tu watazitumia vyema mechi zao za mwisho zinazochezwa mwishoni mwa wiki hii, ambapo Simba itaikaribisha AS Vita wakati Al Ahly itakuwa mwenyeji wa JS Saoura mjini Alexandria, Misri.
Kutokana na hali hiyo bado tunaamini Simba kama itaendeleza ule umwamba wake wa kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya AS Vita basi tiketi ya robo fainali itawahusu safari hii, kwani endapo itashinda, itafikisha alama tisa zitakazowapa moja ya nafasi ya kusonga mbele.
Kwani endapo JS Saoura itaifunga Al Ahly itafikisha alama 11, lakini kama mechi hiyo ya Misri itaisha kwa sare maana yake JSS itafikisha alama tisa na Al Ahly nane, hivyo kuamua timu moja wapo kuungana na Simba.
Kwa namna yoyote Simba inahitajika kushinda tu nyumbani ili kuendeleza rekodi zake na kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kuvuka makundi ya Ligi ya Mabingwa ama Kombe la Shirikisho Afrika kwenda robo fainali. Haijawahi kutokea tangu mfumo wa sasa wa michuano ya CAF iliyobadilika mwaka 1997 na 2004. Hivyo kwa namna yoyote hakuna kitu kingine ambacho Simba inatakiwa kufanya Jumamosi ijayo kwenye kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ila kupata ushindi dhidi ya AS Vita, kwani bado nafasi kwao ipo ya kuvuka kutoka Kundi D.
Hata hivyo, Mwanaspoti bado linaamini Simba haipaswi kushuka uwanjani kinyonge dhidi ya Vita ama kujiamini kupita kiasi kwa kurejea matokeo yao ya nyuma ya mechi za nyumbani, bali ishuke ikiwa imejiandaa kukabiliana kiume na wapinzani wao na kupata matokeo wanayotaka.
Kuna wakati timu zinapojiamini kupita kiasi, hujikuta wakiangukia pua kwa vile huwa hazijui timu zinazocheza nazo zimejiandaa vipi. AS Vita sio timu ya kubezwa kwani ikiwa kwao iliisasambua Simba kwa mabao 5-0, hivyo kuonyesha kuwa kama Simba itaamini itawapiga kirahisi, inaweza kuwakuta yale ya mwaka 1993 katika fainali za Kombe la CAF dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Baada ya sare ya 0-0 ugenini, Simba iliamini ingeshinda kirahisi mchezo huo na kubeba taji la kwanza la Afrika, lakini kilichotokea ilikuwa ni fedheha kwao na Rais wa kipindi hicho, Ali Hassan Mwinyi kwani, Wekundu wa Msimbazi walipigwa mabao 2-0 na kuwaacha wageni wakiondoka na taji. Wachezaji wa Simba lazima watambue kuwa matokeo mazuri sio tu yatarejesha furaha kwa mashabiki wa klabu hiyo na watanzania wengine wanaofuatilia soka, lakini pia itaipa timu yao nafasi ya kuandikisha rekodi itakayokuja kudumu kwa muda mrefu na kuwapa heshima wao.
Hakuna timu ya Tanzania iliyowahi kuvuka na kucheza robo fainali au hatua nyingine za juu za michuano ya CAF tangu mifumo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kubadilishwa kwani mara zote klabu hizo wawakilishi zimekuwa zikishia makundi tena kwa aibu.
Kwa hali na rekodi hiyo ni lazima nyota wa Simba wawakabili Wakongo kama mbogo aliyejeruhiwa kwa nia ya kuhakikisha katika mchezo huo wanapata ushindi Jumamosi. Itakuwa ni aibu kwao kama itakubali Vita iwafunge tena nyumbani baada ya kuwadhalilisha katika mechi ya kwanza ugenini. Tunaamini Simba ina kikosi kizuri, ila makosa madogo yamekuwa yakiigharimu katika mechi zao zilizopita hasa kwenye safu yao ya ulinzi, kitu ambacho Kocha Patrick Aussems atarekebisha mapema kabla ya mchezo huo wa Jumamosi. Nafasi ya Simba kufuzu ama kutofuzu robo fainali ipo mikononi mwa wanasimba na hasa wachezaji katika kuhakikisha wanaiduwaza AS Vita.