Gomes: Banda asainishwe

KOCHA wa Simba, Didier Gomes tayari amepitisha majina ya wachezaji wawili wa kigeni ambao uongozi wa timu hiyo unatakiwa kuhakikisha kabla ya dirisha la usajili kufungwa Agosti 31, wanasaini.

Mmoja wao ni Mmalawi Peter Banda kutoka Sheriff Tiraspol ya nchini Moldova na mwingine ambaye bado wanafanya siri kubwa.

Inaelezwa kwa kiasi kikubwa mazungumzo ya Banda ni kama yamekwisha na kilichobaki ni kusaini mkataba huo wa Simba na jambo hilo linafanyika kwa uharaka kwani ni mapendekezo ya kwanza ya Gomes aliyepo likizoni kwao Ufaransa.

“Banda ndio mchezaji wa kwanza wa kigeni msimu huu kusajiliwa na Simba na haya ndio mapendekezo ya Gomes kabla ya kuondoka kwenda kwao kwa ajili ya likizo,” kilisema chanzo chetu cha uhakika.

Inaelezwa Gomes amewapatia Simba straika mwingine matata mwenye uwezo wa kufunga lakini jina lake halikupatikana kwa haraka na huyo atakuja kuchukua nafasi ya Meddie Kagere ambaye huenda akatolewa kwa mkopo.

Mmoja wa vigogo wa Simba, alisema unajua hawana nafasi ya kusajili mchezaji wa kigeni hadi wateme walionao wakati huu kwani wapo kumi kama kanuni zinavyowataka.

“Uamuzi wetu Chikwende ataenda kwa mkopo na nafasi yake ndio atachukua Banda, baada ya hapo tunataka kiungo anayeweza kucheza namba nane na mwenye sifa zaidi, huyo atakuja kuchukua nafasi ya Luis Miquissone ambaye kuna asilimia kubwa ni kumuuza,” alisema kigogo huyo na kuongeza;

“Kuna wenzetu tayari wapo na jina la huyo straika ambaye Gomes amempendekeza na wanapambana ili kuona jinsi gani watampata na tukifanikiwa atakuja kuchukua nafasi ya Kagere,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa mpango wa msimu ujao ni kuwekeza zaidi kwa upande wa kusajili wachezaji wazuri bila kujali gharama.