Gomes achomoa ofa ya Waarabu

Saturday May 01 2021
gomes pic
By Mwandishi Wetu

MASHABIKI wa Simba hawana sababu ya kuwa na presha kutokana na kuwepo kwa taarifa kwamba kocha wao, Didier Gomes anatakiwa na Libya ili kwenda kuinoa timu yao ya taifa, kwani Mfaransa huyo amesema hana mpango wa kusepa Msimbazi licha ya ofa hiyo ya taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Kocha Gomes ni miongoni mwa makocha wanane waliotajwa kupendekezwa na Chama cha Soka cha Libya ili kuchukua nafasi ya Zoran Filipovic, lakini akizungumza jana na Mwanaspoti alisema hawezi kujadili ishu za mtandaoni, huku akisema yeye ni mwajiriwa wa Simba kwa sasa.

Kupitia kituo cha runinga nchini Libya cha Alahrar Tv kilitoa taarifa kuwa Gomes ni miongoni mwa makocha wanaopendekezwa kwenda kukifundisha kikosi hicho cha Waarabu, wengine wakiwa ni

Javier Clemente, Hector Cuper, Sebastien Desabre, Hubert Velud na Hossam Hassan.

Mwanaspoti lilimsaka Gomes jana na kuzungumza naye juu ya taarifa hizo alizokiri ameziona, lakini yeye bado ana mkataba na Simba na hafikirii kuondoka katika kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara.

“Mimi ni kocha wa Simba kwa sasa na sina mpango wa kuondoka hapa, kwani napata kila kitu changu kwa wakati. Nafikiria kuwa hapa kwa miaka mingi zaidi,” alisema Gomes anayetimiza siku 97 leo tangu aanze kuinoa Simba, Januari 24, mwaka huu akitokea Al Merrikh ya nchini Sudan.

Advertisement

Kocha huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuinoa timu hiyo na kuiwezesha kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa mechi zake kuanzia Mei 14-22 ili kusaka timu za kucheza nusu fainali.

Sambamba na kimataifa, kocha huyo ameiwezesha timu hiyo kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 61 kwa sasa.

Advertisement