Gomes abadili kikosi, Simba ikiikabili Lyon

New Content Item (2)
New Content Item (2)

WACHEZAJI wa Simba ambao hawakupata nafasi katika mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly wanatarajiwa kupewa nafasi kubwa ya kuanza mechi ya leo dhidi ya African Lyon.

Simba inashuka kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa saa 1:00 jioni leo Ijumaa ya Februari 26,2021 ikiwa ni mchezo mtoano wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kupitia kwenye mtandao wa Simba wa kijamii (Instagram), kocha  wao Didier Gomes amesema lengo lake ni kutaka wachezaji wengine waonyeshe uwezo wao kwa mashabiki pia kuwapumzisha wale ambao walicheza dhidi ya Al Ahly.

"Tunawapa nafasi wachezaji wengine waonyeshe mashabiki kwamba wapo vizuri, pia kutoa nafasi ya kuwapumzisha wachezaji waliocheza mchezo wa Al Ahly, sababu wanahitaji kupumzika," amesema.

Amesema lengo lake ni kuona wanafanya vizuri CAF, ASFC na Ligi Kuu Bara, hivyo kila mchezaji anataka apambane kwa kadri anavyoweza kuisaidia timu kupata ushindi.

Simba inashuka uwanjani ikiwa na morali ya hali ya juu baada ya Jumanne ya wiki hii kuwafunga bao 1-0 Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kujizolea pointi sita kwa michezo miwili iliyocheza mpaka sasa ikiwemo ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita ya DR Congo.

Kikosi kilichocheza dhidi ya Al Ahly mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kipa Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Joash Onyango, Pascal Wawa, Taddeo Lwanga, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Chriss Magalu, Luis Miquissone, Hassan Dilunga.

Ambao  walikaa benchi  na waliingia kucheza ni Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Larry Bwalya, Francis Kahata, Meddie Kagere ambapo Benard Morrison na Beno Kakolanya hawakucheza.