Gael, Yanga ngoma mbichi

KIUNGO Mrundi Gael Bigirmana ameikalia kooni Yanga akitaka impe barua ya kuondoka na kumlipa mamilioni ya pesa baada ya kile alichodai kukiukwa kwa vipengele vya mkataba.

Sakata la mchezaji huyo lilianza usajili wa dirisha dogo ulilofungwa Januari 15, mwaka huu, ambapo Yanga ilimnyofoa Ligi Kuu na nafasi yake kumpa beki Mmali Mamadou Doumbia na kutimiza majina 12 ya mastaa wa kigeni.

Hata hivyo, Yanga ilimbakisha Gael kwenye usajili wa CAF, jambo ambalo kwa mujibu wa mmoja ya vigogo wa timu hiyo (jina tunalo), bado ni mchezaji wao kwani nyota huyo wa zamani wa Newcastle United ya Ligi Kuu England alisaini mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa msimu huu.

Suala hilo lilimlazimu Wakala wa Gael, Costantine Mutima kutoka England anakoishi kuja kuongea na viongozi wa Yanga akitaka maelezo ya kina lakini hadi sasa hakuna kilichoeleweka.

Mutima alizungumza na Rais wa timu hiyo, Hersi Said na Mtendaji Mkuu, Andrew Mtine ili kumaliza jambo hilo lakini inaelezwa mazungumzo hayakuwa na majibu ya moja kwa moja baada ya wakala huyo kutaka Yanga imlipe Gael asepe zake.

Inaelezwa Yanga iliendelea kutotoa ushirikiano wa kutosha kwa wakala huyo aliyekuwa amepanga kuondoka nchini na mchezaji wake mwanzoni mwa wiki hii, ndipo akaamua kuandika barua TFF akitaka uthibitisho wa usajili wa Gael kisha afuate hatua za kisheria ikiwemo kwenda Fifa.

Mwanaspoti linajua Gael ameingiziwa mshahara wa Januari na Yanga na bado yupo nchini akitarajia kuondoka siku yoyote kuanzia Jumatatu ijayo.

Mutima alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo alisema Yanga haijampa jibu la moja kwa moja na muda unaenda kwani mteja wake hana furaha kikosini hapo.

“Ni kweli tumewaandikia TFF tukitaka watupe uthibitisho wa usajili na baada ya hapo tutafuata hatua nyingine za kisheria,” alisema.

Gazeti hili lilimpigia simu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred kidao lakini hakupokea, likamtafuta Mkuu wa Kitengo cha Habari na Masoko cha shirikisho hilo, Boniface Wambura ambaye alielekeza apigiwe Ofisa Habari, Cliford Ndimbo ambaye naye aliomba muda.