Fred Vunjabei aula Simba, aweka Sh2 bilioni kutengeneza jezi

#LIVE​: MKUTANO WA SIMBA NA WANAHABARI

Muktasari:

Mfanyabiashara Fred Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei ameshinda tenda ya kutengeneza jezi na vifaa vya michezo vya Simba kwa mkataba wa miaka miwili yenye thamani ya Sh 2 bilioni.

Mfanyabiashara Fred Ngajiro maarufu kama Fred Vunjabei ameshinda tenda ya kutengeneza jezi na vifaa vya michezo vya Simba kwa mkataba wa miaka miwili yenye thamani ya Sh 2 bilioni.

Mtendaji mkuu wa Klabu ya Simba, Barbara Gonzalez amesema Fred ameshinda tenda hiyo baada ya kushindanishwa na makampuni 11 kutoka nchi mbalimbali.

Barbara amesema mchakato wa kupata kampuni itakayotengeneza jezi pamoja na vifaa mbalimbali  vya michezo vya Simba ulianza Desemba mwaka jana ukihusisha makampuni makubwa Duniani.

"Mwaka iliopita aliyepata tenda hii aliweka Sh 100 milioni lakini Fred ameongeza thamani kubwa na kuweka Sh 2 bilioni ni jambo kubwa sana na inaonyesha jinsi Simba ilivyo klabu kubwa.

"Tenda hiyo haihuishi jezi tu bali vifaa mbalimbali kama kofia, barakoa, skafu na vingine vingi hivyo tunaamini mashabiki wetu wataamuunga mkono, " amesema Barbara.

Naye Fred Vunjabei ameishukuru Simba kwa kumwamini na kumpa tenda hiyo huku akiahidi kutoa vifaa vyenye ubora mkubwa.

"Nashukuru Simba kuwa kuniamini kama kijana na mtanzania ambaye nilikuwa nashindana na makampuni makubwa kutoka nje, ikiwemo Afrika Kusini.

"Licha ya kushinda kutengeneza jezi na vifaa vya michezo pia Simba wametupa mamlaka ya kusimamia matukio yote ya klabu hiyo," amesema Vunjabei.

Kwa upande wa msanii wa Hipo Hop, Profesa J amesema Simba inafanya mambo ya makubwa ambayo yanapaswa kuungwa mkono na Watanzania ambao wanapenda maendeleo.

"Yanga wanafaa kuiga mfano huu wakuwa na wawekezaji mbalimbali ambao watafanya soka liwe  na ushindani wa hali ya juu, ambao itasaidia wachezaji kunufaika na vipaji vyao,"amesema.


MANENO YA MANARA

Msemaji wa Simba, Haji Manara amesema Simba ni ‘next level’ kutokana na uwekezaji wa jezi ambao haijawahi kutokea kuwa na thamani hiyo.

"Simba tunawapa furaha mashabiki kuanzia uwanjani hadi katika uwekezaji ina thamani kubwa,"amesema.