Prime
Fadlu apanga mkakati mzito Kwa Mkapa

Muktasari:
- Mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, Simba iliotoka sare ya 1-1, uliwafanya vijana hao wa Fadlu kutinga hatua hiyo baada ya kufikisha pointi 10 katika kundi A nyuma ya CS Constantine wenye pointi 12 huku ikiwa imesalia raundi moja kutamatisha hatua ya makundi na itacheza wikiendi hii nyumbani dhidi ya CS Constantine.
KOCHA wa Simba SC, Fadlu Davids ameweka wazi timu yake inajivunia kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini amesisitiza bado wanakusudia kufanya jambo wakiwa Kwa Mkapa.
Mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, Simba iliotoka sare ya 1-1, uliwafanya vijana hao wa Fadlu kutinga hatua hiyo baada ya kufikisha pointi 10 katika kundi A nyuma ya CS Constantine wenye pointi 12 huku ikiwa imesalia raundi moja kutamatisha hatua ya makundi na itacheza wikiendi hii nyumbani dhidi ya CS Constantine.
“Tulikuwa na malengo ya kufuzu mapema na sasa tumefanikiwa. Lakini bado kuna jambo moja muhimu na hilo ni kumaliza kileleni mwa kundi letu,” alisema kocha Fadlu na kuongeza.
“Mchezo dhidi ya CS Constantine ni muhimu sana kwetu, ni mchezo wa kutafuta pointi tatu zitakazokaa na kutufikisha kwenye kilele cha kundi.”
Kocha huyo pia alizungumzia changamoto zinazoweza kujitokeza katika mchezo huo wa Jumapili dhidi ya CS Constantine, ambayo ameisema ni mojawapo ya timu ngumu zaidi walizokutana nazo katika hatua hii ya makundi ambapo kwenye mchezo wa kwanza walipoteza kwa mabao 2-1.
“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu CS Constantine ni timu nzuri na wanajua kucheza mechi kubwa,” alisema Fadlu na kuongeza.
“Tutahitaji kuwa makini na kujitahidi kuvunja ulinzi wao, lakini tuna uwezo wa kushinda kama tutakuwa na mchezo wetu wa kushambulia na kumiliki mpira.”
Akizungumzia umuhimu wa mashabiki, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisisitiza ni msaada wao utakuwa na muhimu mkubwa sana kwa timu, na aliwashukuru kwa kuendelea kuwa na timu.
“Mashabiki wetu wamekuwa bega kwa bega nasi tangu mwanzo na naomba waje kwa wingi Jumapili kujaza uwanja wa Benjamin Mkapa. Tunaahidi tutapigania kila pointi kwa ajili yao,” alisema kocha huyo.
Simba imefuzu robo fainali ya sita kati ya saba katika michuano ya CAF tangu msimu wa 2018-2019.
Akiongelea mafanikio hayo, kocha wa zamani wa wekundu hao wa Msimbazi, Patrick Aussems amewapongeza na kuwatakia kila la kheri katika hatua inayofuata.
“Kila kitu kipo mikononi mwao, wana nafasi ya kufanya vizuri zaidi kikubwa ni kuendelea kuwa pamoja na kupigania mafanikio,” alisema.
Aussems aliiongoza Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huo na walitolewa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya michezo miwili.
Wakati huo huo, kipa namba moja wa Simba, Moussa Camara alisema hesabu zao za kumaliza kundi kinara zina umuhimu mkubwa kwani itawasaidia hatua ya robo fainali kuanzia ugenini na kumalizia nyumbani.
“Tumefuzu kweli lakini tuna hesabu zingine kama mbili, kwanza tunataka kushinda hii mechi ya mwisho dhidi ya Constantine ili tuongoze kundi letu jambo ambalo litatupa faida huko tunakokwenda.
“Endapo tukifanikiwa kushinda tutacheza mechi za robo fainali tukianzia ugenini na kumalizia nyumbani, kama mnavyoona hakuna timu ambayo imefanikiwa kuondoka hata na pointi moja tukiwa nyumbani hii ina maana tutapata nafasi ya kuja kumalizia vizuri mchezo wa robo na hata kwenda nusu fainali,” alisema Camara na kuongeza.
“Hatusahau kwamba hii ni timu ambayo ilitufunga kwao, hakuna timu nyingine iliyoondoka na pointi tatu dhidi yetu, tunataka kusahihisha makosa yetu, walipata ushindi ule kwa makosa yetu, tutakuwa nyumbani kusahihisha makosa yetu mbele ya mashabiki wetu.”