Eti Pep hamuuuzi Foden hata kwa Euro 500m

Muktasari:
Na kocha Guardiola anaamini kwamba Foden, 19, ni silaha ya baadaye ya Man City, kwamba atakuwa ‘mchawi’ wao wakati David Silva atakapoachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND. PEP Guardiola amedai kwamba Phil Foden ndiye mchezaji pekee kwenye kikosi cha Manchester City ambaye hatauzwa hata uweke mezani mkwanja wa Euro 500 milioni.
Kinda huyo Mwingereza ameamua kutuliza maisha yake kwenye klabu hiyo licha ya kwamba amekuwa hapati nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Na kocha Guardiola anaamini kwamba Foden, 19, ni silaha ya baadaye ya Man City, kwamba atakuwa ‘mchawi’ wao wakati David Silva atakapoachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu.
Guardiola alisema: “Hatukumpa tu Foden mkataba mpya kwa bahati mbaya. Huyu ni mchezaji pekee ambaye hatuwezi kumuuza katika mazingira yoyote yale, ni yeye pekee. Hauzwi hata kwa Euro 500 milioni,” alisema.
“Phil haendi kokote — Phil ni Man City. Hatuwezi kumsajili mtu mwingine yeyote kwenye nafasi hiyo. David Silva atakapoondoka, basi Phil atakuwa mchawi wetu.”
Man City hawataki kufanya uzembe kama walivyofanya huko nyuma, walipomruhusu Jadon Sancho aende Borussia Dortmund na Brahim Diaz kwenda Real Madrid, ambapo huko wamekuwa kwenye viwango bora na msaada kwa timu zao.
Lakini, Guardiola anaaminni Foden ni fundi zaidi wa mpira kuliko makinda hao wengine wawili - Sancho na Diaz.