Enekia apata dili Saudia Arabia

NYOTA wa kimataifa wa soka la wanawake nchini, Enekia Kasongo amepata dili la kujiunga na timu ya Eastern Flames FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Saudia baada ya mchongo wa kwenda Ukraine kukwama.

Awali, Enekia alikuwa kwenye hatua nzuri ya kusaini mkataba na Kryvbas Womens Team ya Ukraine, lakini dili hilo lilikwama kutokana na kuchelewa kwa viza, ndipo menejimenti ya nyota huyo ikajiongeza Saudia.

Mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo alisema Enekia tangu juzi amefaulu vipimo vya afya na muda wowote atakamilisha usajili wa msimu mmoja.

Alisema Enekia atajiunga na timu hiyo akimaliza majukumu ya timu ya taifa ‘TwigaStars’ kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake huko Morocco mwezi huu ikianza na Ivory Coast.

“Ni kweli Enekia alikuwa kwenye hatua nzuri kujiunga na timu ya Ukraine lakini ilikwama kwa sababu tulichewa kushughulikia (viza) tukaona tumtafutie timu mapema ili acheze,,” alisema mtu huyo aliyeomba asitajwe jina. Eastern Flames FC ndio timu ya kwanza kwa wanawake kuanzishwa Saudi Arabia 2006 na inatumia Uwanja wa Prince Mohamed bin Fahd, ikishinda Ligi ya Kanda ya Mashariki mara mbili mfululizo 2020 na 2021.