Dk Devotha kutetea kiti chake Chaneta

Wednesday October 13 2021
NETBAL PIC

Dk Devotha Marwa

By Imani Makongoro

Dk Devotha Marwa amefichua kutetea kiti chake kwenye uchaguzi mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta).

Mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake atachuana na wagombea wengine wawili waliojitosa kuwania nafasi hiyo.

SOMA: Dk Devotha: Najuta kugombea Chaneta

Hata hivyo Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeeleza kutoweka wazi wagombea hao hadi wakati muafaka uliopangwa utakapowadia.

"Wamejitokeza wagombea kama 20, nafasi ya mwenyekiti wapo watatu na nafasi nyinginezo, lakini muda wa kutoa majina bado," amesema Najaha Bakari ofisa michezo wa BMT.

SOMA: Dk Devotha amrithi Kibira Chaneta

Advertisement

Ingawa Dk Devotha ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amefichua kuchukua fomu kutetea kiti chake kwenye uchaguzi wa Jumamosi utakaofanyika mjini Dodoma.

"Sifahamu nachuana na nani kwenye nafasi hiyo, lakini tayari nimechukua na kurejesha fomu ya kutetea kiti changu," amesema Dk Devotha ambaye huu ni msimu wake wa pili kugombea Chaneta tangu 2017  alipichukua kijiti cha Anna Kibira (sasa ni marehemu).

Wagombea wote watafanyiwa usaili Ijumaa ijayo mjini Dodoma tayari kwa uchaguzi huo.

"Mchakato wa uchaguzi unakwenda vizuri, majina ya wagombea tutayatangaza siku moja kabla ya usaili," amesema Najaha.

Katibu anayemaliza muda wake, Judith Ilunda pia inaelezwa amechukua fomu ya kutetea kiti chake akitarajiwa kupewa ushindani na Edson Chatanda kocha wa Polisi Morogoro.

Mchakato wa kurudisha na kuchukua fomu ulifungwa jana saa 12 jioni.

Advertisement