Dk Devotha: Najuta kugombea Chaneta

Muktasari:

Mwenyekiti huyo alisema uamuzi wa kuingia Chaneta haukuwa sahihi ingawa alikuwa na nia njema ya kuleta maendeleo katika mchezo wa netiboli ambao umedorora.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Dk Devotha Marwa amesema alikosea kuwania uongozi ndani ya taasisi hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, mwenyekiti huyo aliyerithi mikoba ya Anna Kibira alisema ameshindwa kutimiza ndoto yake licha ya kudumu madarakani kwa miaka mitatu.

Dk Devotha alisema katika muda huo amekuwa akitumia fedha zake za mfukoni kwa kazi za chama, hivyo hatagombea tena katika uchaguzi ujao wa mwezi Desemba, mwaka huu.

Mwenyekiti huyo alisema uamuzi wa kuingia Chaneta haukuwa sahihi ingawa alikuwa na nia njema ya kuleta maendeleo katika mchezo wa netiboli ambao umedorora.

“Kulia ada ya Shirikisho la Dunia IFNA Dola 888 nilitumia fedha yangu na Waziri Jafo (Selemani) alichangia milioni mbili achilia mbali ile ya Shirikisho la Afrika Dola 250. Naona kama nilikosea kuwa kiongozi wa Chaneta,”alisema Dk Devotha.

Alisema waliposhindwa kupeleka timu katika mashindano ya Afrika nchini Afrika Kusini, alitumia fedha zake kuhudhuria mkutano mkuu wa Afrika uliotumika kuirejeshea Tanzania uanachama.

Mwaka 2012 timu ya Taifa, ‘Taifa Queens’ ilitwaa dhahabu katika michezo ya Afrika na 2011 ilitwaa fedha katika All African Games. Tanzania iliwahi kushika nafasi ya tatu kwa ubora Afrika na 13 duniani chini ya aliyekuwa mwenyekiti Anna Bayi.