Diarra aukubali mziki wa Kagere

KIPA wa Yanga, Diarra Djigui ‘Screen Protector’ amekiri kuwa licha ya kukutana na washambuliaji wakali katika mechi tisa za Ligi Kuu Bara, huku sita akicheza bila kuruhusu bao, hakuna aliyemnyima raha langoni kama straika wa Simba, Meddie Kagere.
Diarra alisema katika mechi zote za ligi Kagere ndiye mshambuliaji wake bora zaidi kwenye ligi hiyo iliyoingia raundi ya 10.
Kipa huyo kutoka Mali, aliliambia Mwanaspoti kuwa Kagere ni hatari zaidi kwa sababu muda mwingi hukaa kwenye nafasi ambazo mpira ndio huangukia ama kupita.
“Yule mshambuliaji wa Simba (Kagere) ndiye mshambuliaji hatari, kwani utamuona mbele ya lango kwenye nafasi sahihi, jambo ambalo ni hatari zaidi kama kipa hawi makini, kwani anaweza kufunga muda wowote na hata tulipocheza naye alininyima raha kwa kuhofia angetutibulia,” alisema Diarra aliyesajiliwa kutoka klabu ya nchini kwao Stade Malien aliyefungwa mabao matatu tu katika ligi.
Mbali ya kumzungumzia Kagere, Diarra pia alizungumza utofauti wa Ligi Kuu Bara na ile ya kwao na kusema Tanzania ni ngumu kwa aina ya ratiba, huwa haiwapi wachezaji muda mwingi wa kupumzika.