Daktari aitungia shairi Taifa Stars

Muktasari:
- Taifa Stars imefuzu fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 1980.
Dar es Salaam. Daktari wa Wilaya ya Itilima, Beatus Chikoti ametunga shairi maalum la kuisifia timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' baada ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri mwezi Juni.
Stars ilijihakikishia tiketi yake ya AFCON baada ya kuibanjua Uganda kwa mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho wa kundi L uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Kutokana na matokeo ya Cape Verde kutoka sare ya bila kufungana, Stars iliungana na Uganda kusonga mbele kwani ilifikisha pointi nane katika mechi zote sita za kundi hilo.
Katika shairi lake, Dokta Chikoti ameifananisha Stars na mdudu Kakakuona ambaye amekuwa haonekani mara kwa mara
KAKAKUONA KONGOLE
1. Miaka thalatha kenda, mwaka huu imetimia
Tokea uliposhinda, na ukafuzu sawia
Hatimaye ukaenda, nchini Naijeria Kakakuona kongole,
kuweka historia.
2. Miaka arobaini, kimsingi nakwambia
Tino aliposaini, kwenye lango la Zambia
Juzi Msuva na Nyoni, nao wakairudia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
3. Agirei wa Morisi, ushindi kapalilia
Kwa uchu mithili fisi, kichwa alipigilia
Tukafurahi na sisi, heshima kujipatia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
4. Jella Mtemi na Tenga, ujana wakumbukia
Shindanoni walitinga, nchi wakapigania
Shabaha wakailenga, jambo hilo kurudia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
5. Ilibidi kusubiri, kwa miongo tukilia
Tulikosa ujasiri, wengine kuwatambia
Ama tulitahayari, kwa vichapo kuchezea
Kakakuona kongole, kuweka historia.
6. Mbwana Ali Samatta, nahodha alotimia
Beji alipofumbata, moyoni alinuia
Kufuzu tupate pata, na hilo limetimia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
7. Ukuta ule imara, hakika umetulia
Mbaga hana masihara, Yondani na Kessy pia
Hawakuwa na papara, ulinzi kusimamia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
8. Boko ni mpiganaji, jemedari asilia,
Faridi naye kipaji, Mudathiri ana nia
Manula mtia chaji, na mikwaju kuzuia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
9. Fei Toto ni mahiri, pindi anapoingia
Wengine wote hodari, nchi wametumikia
Kapombe aliumia, naye pia askari
Kakakuona kongole, kuweka historia.
10. Amunike namsifu, heshima katuletea
Mkali kama siafu, nidhamu kasimamia
Heko kwa tiefuefu, na ile kamati pia
Kakakuona kongole, kuweka historia.
11. Rais nakupongeza, morali uliwatia
Na sasa umeongeza, viwanja kuwapatia
Hakika inapendeza, kwa sote watanzania
Kakakuona kongole, kuweka historia.
12. Kakakuona geuka, na ushindi dumishia
Usije kuadimika, kwa miongo kupotea
Misri kapige soka, tuzo zipate tujia
Kakakuona kongole, kuweka historia.