Dakika 180 zampa faraja David Ouma

Muktasari:
- Singida imecheza mechi hizo mbili kwa kuanza na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kutoka sare ya 2-2 zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati Manyara, ikiwa ni za kutesti mitambo kabla ya kurejea katika mechi za Ligi Kuu inayoendelea mapema wiki ijayo baada ya kumalizwa viporo.
BAADA ya kucheza dakika 180 dhidi ya Fountain Gate katika mechi mbili za kirafiki, kocha mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema ataendelea kusaka mechi zaidi kujiweka tayari kuikabili Simba katika mechi mbili mfululizo ikiwamo ya Ligi Kuu na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (FA).
Singida imecheza mechi hizo mbili kwa kuanza na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kutoka sare ya 2-2 zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati Manyara, ikiwa ni za kutesti mitambo kabla ya kurejea katika mechi za Ligi Kuu inayoendelea mapema wiki ijayo baada ya kumalizwa viporo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema ana dakika 180 ngumu kusaka pointi mbele ya Simba kwenye mechi mbili za mashindano wakitarajia kukutana hatua ya nusu fainali Kombe la Shirikisho (FA) Mei 31 na mechi ya ligi Mei 28.
“Hatuna ratiba ya kucheza mechi yoyote hapa katikati hadi tutakapokutana na Simba ambayo bado inaendelea kucheza mechi za ligi na Kombe la Shirikisho Afrika ili kuendana na kasi hiyo tunahitaji muda wa kucheza zaidi na ndio maana nasema nitakuwa na mechi nyingine za kirafiki,” alisema na kuongeza;
“Sijajua nitacheza na timu gani ila nimeomba viongozi wanitafutie mechi zaidi na naamini mambo yataenda vizuri kwa sababu mikakati ni kutinga hatua inayofuata Kombe la FA lakini pia kukusanya pointi zaidi za ligi ili kukimbizana na mshindani wetu Azam tukiwania nafasi ya tatu kwenye msimamo.”
Ouma akizungumzia dakika hizo 180 dhidi ya Simba alisema ratiba sio rafiki sana lakini wanapambana kujiweka fiti ili waweze kufikia malengo yao na amebainisha kuwa wanakutana na timu ngumu lakini anafurahishwa na ubora wa nyota wake.