Clatous Chota Chama : Yaani warembo kila kona, aingizwa mjini

Muktasari:
Tukio hilo mbali na kuzungumzwa na mashabiki wengi wa soka akiwemo tajiri Mohammed Dewji ‘Mo’, kwa Chama limeshapita na ameshasahau ingawa katika maisha ya mwanadamu litabaki kuwa kumbukumbu. “Ahaaa! Ishu ya bao imeshapita ile, kwa sasa naangalia mbele, mambo yanapopita inakuwa imekwisha na sasa tunaanza upya.” anasema.
UKISIKIA mwamba wa Lusaka kwa Tanzania huwezi kujiuliza mara mbili anayetajwa ni nani kwa sababu wadau wa soka watajua tu ni Cletus Chota Chama anayevaa jezi namba 27 ndani ya kikosi cha Simba.
Jina hilo ni kwa sababu jamaa huyo ni mzaliwa na mwenyeji wa Zambia, nchi ambayo mji mkuu wake ni Lusaka, lakini asili ya mchezaji huyo ni Mufulira ikiwa ni wilaya maarufu kwa uchimbaji madini ya shaba na ipo mpakani mwa DR Congo. Chama amezaliwa Mufulira, lakini anakoweka makazi ni Ndola.
Chama anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, lakini kutokana na uwezo wake wa kupachika mabao na upungufu wa washambuliaji ulio katika kikosi hicho kwa sasa, Kocha wa Simba Mbelgiji Patrick Aussems amekuwa akimchezesha kama mshambuliaji wa pili au winga wa kulia na au kushoto.
Alijizolea umaarufu zaidi kutokana na bao alilowafungia Simba dakika za lala salama katika mchezo wao dhidi ya Nkana ya Zambia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Bao hilo ndilo liliwapeleka kucheza hatua ya makundi ya mashindano hayo msimu wa 2018-2019.
Bao hilo liliingia ndani ya dakika za nyongeza baada ya zile 90 za mchezo kumalizika huku mashabiki wa Simba wakiwa tayari wameanza safari ya kwenda majumbani kwao wamekata tamaa na wengine hawajui cha kufanya.
Tukio hilo mbali na kuzungumzwa na mashabiki wengi wa soka akiwemo tajiri Mohammed Dewji ‘Mo’, kwa Chama limeshapita na ameshasahau ingawa katika maisha ya mwanadamu litabaki kuwa kumbukumbu. “Ahaaa! Ishu ya bao imeshapita ile, kwa sasa naangalia mbele, mambo yanapopita inakuwa imekwisha na sasa tunaanza upya.” anasema.
MADEMU KILA KONA
Kuna maneno ya mtaani kuwa sehemu ya mastaa waliovamia jiji hasa wachezaji hujikuta wakishindwa kutimiza wajibu wao wa kucheza mpira baada ya kurubuniwa na wanawake wa aina hiyo. Na wapo wanawake ambao hutumiwa na wachezaji ambao wanawania namba moja kwa ajili ya kuwaharibu wapinzani wao na lengo linapotimia hugeuka na kuaminiwa vikosini.
Chama anakiri wapo mademu wamekuwa wakimsumbua ili watoke naye kimapenzi, lakini anasisitiza hilo ni jambo la kawaida na halipo Dar es Salaam tu, bali ni dunia nzima.
“Unajua suala la staa kutakiwa kimapenzi na mwanamke ni kawaida na hii ipo duniani kote, kwangu mimi sioni kama ni kitu cha ajabu. Kuwapenda watu maarufu ili watoke nao kimapenzi tena unaweza kukuta hata Tanzania kuna unafuu,” anaeleza Chama.
“Inatokea, ni kweli nafuatwa na wanawake wa aina hiyo, lakini hapo inategemea na akili yako mhusika ukubali au ukatae, pia namna unavyolichukulia na kulifanyia uamuzi suala hilo.”
Kiungo huyo anafananisha suala hilo na ilivyo pombe kwa mchezaji. Si kwamba pombe inakatazwa, lakini wapo wanaotumia kinywaji hicho tofauti kwa kunywa kupita kiasi na kutumia katika wakati usio sahihi.
“Wanawake au pombe si wabaya, tatizo linakuwa kwako mtumiaji na matumizi yako. Unafanya kwa mtu sahihi, unakunywa kiasi gani na kwa wakati gani,” anasisitiza Chama ambaye anapenda kuvaa viatu aina ya Nike Mercurialy.
MAAJABU YA UGALI KWA PARACHICHI
Chama anasema, katika maisha yake hapa nchini amegundua wapo watu wana vituko na hasa alipokutana na mtu aliyekuwa akila parachichi.
“Dar es Salaam hii acha kabisa (anacheka sana)! Kuna watu hatari sana, wana vituko mno. Nilikutana na jamaa mmoja anakula ugali kwa parachichi bila mboga. Kwangu niliona kitu cha ajabu kwa sababu sikuwahi kuona maishani mwangu,” anasema Chama.
“Si kama alikuwa na shida isipokuwa alifanya hivyo kwa sababu anapenda na anaona kwake inafaa, sitakuja kusahau kitendo hicho, kwangu ni cha ajabu katika maisha yangu yote tangu nimefika hapa Tanzania.”
MAMBO YA MSOSI
Kiungo huyo ambaye anavutiwa na juisi ya embe pamoja na ile ya kuchanganya matunda mengi (tropico), anasema chakula kinachopatikana hapa nchini na Zambia ni sawa, lakini tofauti ni katika mandaalizi.
“Namna kitakavyopikwa hapa ni tofauti na kule nyumbani kwetu. Lakini, hiyo haimaanishi kuwa cha hapa kinanishinda, nakula bila tatizo maisha yanaendelea,” anasema.
KISWAHILI BAB' KUBWA
Licha ya kuwa Wazambia wanazungumza Kiingereza, kwa sasa Chama anajaribu kuzungumza Kiswahili na mnaelewana.
“Kiswahili najua kidogokidogo, hicho kipo kwa sababu hata kwetu wapo wanaozungumza. Hiki nakiongea, nimejifunza hapa taratibu na awali nilikuwa najua kidogo,” anasema Chama ambaye mara nyingi mbele ya watu amekuwa anazungumza Kiingereza.
MASHABIKI BONGO
Chama anasema amecheza soka katika mataifa tofauti, lakini mashabiki wa Tanzania ni kiboko wanampa raha kutokana na namna wanavyoshabikia timu zao.
“Tanzania si mara ya kwanza kucheza mpira, awali nilijua Simba haina mashabiki wengi lakini baada ya kuwaona ilikuwa furaha, yaani wanapenda sana timu zao jambo linaloleta furaha.”
Anasema kwao amecheza klabu kubwa kama Zesco na Lusaka ambazo zina mashabiki wengi, lakini anaokutana nao hapa nchini hasa Simba ni kiboko.
UJUMBE KWA WANASIMBA
“Kama nilivyosema awali, kilicho mbele yetu hatukijui, kizuri tulifanya maandalizi ya kutosha tulipokuwa Afrika Kusini, imekuwa bahati mbaya tumetolewa ni sehemu ya mchezo, lakini sasa tunajipanga kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine yanayotukabili,” anasema nyota huyo.
“Tuna mipango, tumejiandaa kuona hatufanyi makosa kwa kufanya vizuri kila mchezo, lengo ni kuona tunatetea ubingwa wetu. Pia tunafanya vizuri kwenye FA ili tujipange kwa ajili ya msimu ujao kimataifa Mungu akijalia.”
MAISHA MDANI YA SIMBA
Anasema anafurahia maisha ya Simba kutokana na namna wanavyoishi wachezaji, viongozi pamoja na mashabiki na wanachama.
“Kiujumla ni maisha mazuri, kwanza unaona kama upo nyumbani tu kutokana na namna unavyopokewa, unapata ushirikiano wa kila namna,” anaeleza Chama ambaye ni shabiki wa Barcelona akivutiwa na Lionel Messi.
MAZOEZI BINAFSI
Mafanikio anayopata usifikiri yanapatikana hivihivi tu, jamaa anajituma hasa katika mazoezi na nidhamu kwani achana na matizi wanayofanya pamoja chini ya makocha wao, Chama amekuwa na programu yake binafsi.
“Ni kweli mbali na mazoezi ya timu pamoja na wenzangu, nimekuwa na programu ya mazoezi yangu binafsi na hii si kwamba nafanya kila siku isipokuwa kuna utaratibu maalumu.”
STAILI YA UCHEZAJI
Chama ambaye si muongeaji, ni fundi wa mpira na mzuri zaidi katika umiliki wa kabumbu. Kabla na baada ya kupokea pasi anajua ni mahali gani anatakiwa uelekee, ni mtaalamu wa kupiga pasi za mwisho na pia kupachika mabao.
“Yote ni mipango ya Mungu, kila kitu kinachofanyika huwa inatokea tu yote ni Mungu naweza kusema, lakini pia kujituma, kufuata maelekezo ya kocha na kushirikiana na wenzangu,” anasema mchezaji huyo.
ALIKOTOKEA
Katika maisha ya soka, Chama yuko chini ya uongozi wa Bro Soccer Management. Alizaliwa Juni 18, 1991 na sasa ana urefu wa mita 1.77.
Mkataba wake na Simba unaisha Juni 21, 2020 ukiwa ni wa miaka miwili tangu alipojiunga Julai 1, 2018.
Kabla ya Simba, Chama alizichezea Nchanga Rangers FC, Zesco United FC, Ittehad, Lusaka Dynamos aliyoachana nayo na kujiunga na Lusaka Dynamos.