Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cannavaro amtema Tambwe, amuita Ajibu

Muktasari:

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ametaja kikosi cha wachezaji 11 ambao anaamini ndiyo bora zaidi msimu huu na kuwatosa nyota kadhaa wa timu yake na kuwapa nafasi zaidi wachezaji wengi wa Simba.

YANGA ni bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na Azam ni washindi wa pili, hilo hakuna ubishi.

Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ametaja kikosi cha wachezaji 11 ambao anaamini ndiyo bora zaidi msimu huu na kuwatosa nyota kadhaa wa timu yake na kuwapa nafasi zaidi wachezaji wengi wa Simba.

Cannavaro alisisitiza kwamba wachezaji hao ni kwa mujibu wa utashi wake na ufanisi wao msimu huu bila kujali timu zao zilifanya nini na pia amepanga wazawa.

Kwenye orodha yake amewabania Mrisho Ngassa ambaye ni Mchezaji Bora wa Aprili, kipa wake Ally Mustapha ‘Barthez’, mastraika Amissi Tambwe na Kpah Sherman. Pia amemchinjia baharini staa wa Simba, Emmanuel Okwi.

Cannavaro amewataja wachezaji watano wa Simba, wanne wa Yanga, huku akitoa mmoja mmoja kutoka Mtibwa Sugar, Mbeya City na pia akamtaja kiungo mmoja wa Azam.

Ivo Mapunda

Cannavaro amemtaja kipa wa Simba, Ivo Mapunda kuwa ndiye bora zaidi msimu huu kutokana na uwezo aliouonyesha katika mechi alizocheza. Alisema licha ya umri mkubwa wa Mapunda, amekuwa na kiwango cha juu. Mapunda amefanikiwa kucheza timu mbalimbali nchini na nje ya nchi na kuonyesha kiwango cha kuvutia ambacho kimemshawishi Cannavaro.

Hassan Kessy

Nahodha huyo wa Yanga anaamini beki wa Simba, Hassan Kessy ni miongoni mwa wachezaji wachache vijana nchini wenye uwezo wa juu na wamefanya vizuri msimu huu. Anasema Kessy amekuwa katika kiwango cha juu wakati wote huku pia akionyesha jitihada za kuisaidia timu yake kufanya vizuri. Kessy alisajiliwa Simba akitokea Mtibwa Sugar Desemba mwaka jana.

Juma Abdul

Cannavaro anaamini kuwa Juma Abdul ndiye beki mwingine wa pembeni ambaye amefanya vizuri msimu huu. Amesema ni hodari wa kukaba na kupandisha timu.

Hassan Isihaka

Cannavaro amekwenda mbali na kumtaja nahodha wa Simba, Hassan Isihaka, kuwa anastahili kuwa katika kikosi hiki kutokana na kuthibitisha uwezo wake ndani ya muda mfupi.

Cannavaro anasema licha ya Isihaka kusota katika timu ndogo ndogo kwa muda mwingi bado ameonyesha uwezo wa juu katika msimu wake wa kwanza ligi kuu hadi kupewa unahodha wa timu hiyo.

Kevin Yondani

Cannavaro anaamini beki mwenzake wa kati, Kelvin Yondani ameendelea kuthibitisha uwezo wake msimu huu. Yondani na Cannavaro wamecheza pamoja Yanga na kuiwezesha timu hiyo kutwaa taji la ligi msimu huu.

Jonas Mkude

Nahodha huyo wa Yanga amemtaja Jonas Mkude wa Simba kuwa miongoni mwa viungo bora zaidi msimu huu.

Mkude amefanikiwa kujihakikishia namba katika kikosi cha Goran Kopunovic pia akipata mkataba mpya klabuni hapo uliomfanya kuwa mchezaji ghali zaidi Simba. Anasema kiungo wa Azam, Mudathir Yahya pia anastahili katika kikosi bora.

Simon Msuva

Cannavaro amemtaja mpachika mabao wa Yanga, Simon Msuva kuwa ndiye winga wa kulia aliyefanya kazi yake vizuri zaidi msimu huu na yupo katika kiwango bora zaidi katika maisha yake ya soka.

Said Makapu

Nahodha huyo amemtaja kiungo Said Juma ‘Makapu’ kuwa ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wamecheza msimu wao wa kwanza na kufanya vizuri. Anasema pia nidhamu na usikivu ya kiungo huyo umemfanya kuwa na kiwango cha juu.

Mussa Hassan ‘Mgosi’

Cannavaro anamtaja straika wa Mtibwa Sugar, Mussa Hassan ‘Mgosi’ kuwa ndiye straika aliyemvutia zaidi msimu huu. Anasema ni mchezaji ambaye anaweza kufanya vitu tofauti na wachezaji wengine huku akifanikiwa kucheza kwa misimu kadhaa bila kuchuja.

Ibrahim Ajibu

Cannavaro ameendelea kuvutiwa na wachezaji wa Simba ambapo amemtaja chipukizi Ibrahim Ajibu kuwa anastahili kuwa katika kikosi hichi. Anasema Ajibu ni mzuri mbele ya goli na anaweza kufanya lolote akiwa upande wowote wa uwanja.

Deus Kaseke

Nyota wa Mbeya City, Deus Kaseke amefanikiwa kuingia katika kikosi bora cha Cannavaro.

Anasema chipukizi huyo amefanikiwa kulinda kipaji chake msimu huu sawa na msimu uliopita.

Ameongeza kuwa winga huyo ana kasi inayoweza kumvutia mdau yeyote wa soka.