Camara, Ngoma nusura wazichape New Amaan

Muktasari:
- Tukio hilo lilijiri muda mfupi kabla timu hazijaenda mapumziko, wakati Simba ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
KATIKA hali isiyo ya kawaida, wachezaji wawili wa Simba, kipa Moussa Camara na kiungo mkabaji Fabrice Ngoma, walinaswa wakiwa katika mzozo mkali uliokaribia kugeuka ugomvi wa wazi, wakitaka kuzichapa mbele ya mashabiki kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tukio hilo lilijiri muda mfupi kabla timu hazijaenda mapumziko, wakati Simba ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 dhidi ya RS Berkane katika mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Chanzo cha ugomvi huo kilianza baada ya Simba kuruhusu kona ya mwisho kuelekea mwisho wa kipindi cha kwanza, ambayo ilitokana na Camara kushindwa kumudu mpira wa juu, na kuufanya utoke nje.
Ngoma, ambaye alionekana kuchukizwa na tukio hilo, alimsogelea Camara kwa hasira, akimtuhumu kutokuwa makini.
Ndipo walipokutana uso kwa uso, wakaanza kurushiana maneno makali. Camara naye hakubaki nyuma, akijibu kwa hisia kali, hali iliyowafanya wachezaji hao kuanza kushikana mashati, kitendo kilichosababisha tafrani ndogo katikati ya uwanja.
Wachezaji wengine wa Simba, wakiongozwa na nahodha Mohamed Hussein 'Tshabalala' waliingilia kati kwa haraka kuwatuliza wawili hao, kabla ya mambo kuwa mabaya zaidi. Tukio hilo lilidumu kwa takriban sekunde 40.
Hali hiyo ilionyesha presha kubwa waliyonayo wachezaji wa Simba katika kuwania taji hilo la kimataifa, ambalo ni ndoto ya muda mrefu kwa mashabiki na uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Tukio hilo limezua gumzo miongoni mwa mashabiki waliokuwa wamefurika Uwanja wa Amaan, wengi wakionesha mshangao na wengine wakisema ni dalili ya hasira ya ushindani, huku wakitaka benchi la ufundi kuhakikisha hali kama hiyo haijirudii katika kipindi cha pili.
Ikumbukwe kuwa Simba walikuwa wanahitaji ushindi wa angalau bao moja zaidi kusawazisha matokeo ya mechi ya kwanza waliyoifungwa 2-0 Morocco.
Hadi timu zinakwenda mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Joshua Mutale, baada ya kazi nzuri ya Ellie Mpanzu. Hali ya mchezo ilikuwa ya ushindani mkubwa huku RS Berkane wakionekana kuja na mpango wa kuchelewesha mchezo na kupunguza kasi ya Simba.