Fadlu: Changamoto zimetukomaza, tutarudi kivingine

Muktasari:
- Akizungumza baada ya sare ya 1-1 iliyopatikana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar matokeo yaliyowakosesha Simba taji hilo, alisema timu hiyi ilikabiliana na mazingira magumu kwa ujasiri mkubwa.
KOCHA wa Simba, Fadlu Davids, amesema pamoja na kupoteza nafasi ya kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane, kikosi hicho kimeonyesha ukuaji mkubwa wa kiakili na kimchezo kutokana na changamoto walizokutana nazo kabla na wakati wa fainali hiyo.
Akizungumza baada ya sare ya 1-1 iliyopatikana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar matokeo yaliyowakosesha Simba taji hilo, alisema timu hiyi ilikabiliana na mazingira magumu kwa ujasiri mkubwa.
"Haikuwa tu kuhusu mechi yenyewe, bali hata maandalizi kuelekea mchezo huu yalikuwa na changamoto nyingi. Kutocheza katika Uwanja wetu wa nyumbani (Mkapa) ilikuwa pigo kubwa. Lakini hayo yote yametufanya kuwa imara zaidi," alisema Fadlu.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, aliongeza kuwa mfululizo wa maamuzi yenye utata na faulo ambazo walipewa wapinzani wao kwa urahisi, ziliathiri mwenendo wa mchezo. Hata hivyo, alisifu wachezaji kwa kuonyesha msimamo na nidhamu licha ya presha hiyo.
"Faulo nyingi zilitolewa kwao mara tu zilipotokea, hali hii iliwapa faida RS Berkane kisaikolojia. Halafu ikaja changamoto ya kadi nyekundu kwa Kagoma, lakini hata baada ya hilo, wachezaji wangu hawakukata tamaa," alisema.
Fadlu alisisitiza pamoja na kuondolewa kwa maumivu, Simba imejifunza mengi yatakayowasaidia kuwa bora zaidi katika mashindano yajayo.
"Naipa pongezi kubwa timu yangu. Wamekua sana kupitia mechi hii na mazingira magumu haya. Ni dhahiri tutarudi tukiwa bora zaidi. Changamoto hizi zimejenga uimara mpya ndani yao huu ni msingi wa mafanikio yetu yajayo," aliongeza Fadlu kwa kujiamini.
Fadlu alihitimisha kwa kusema wanahitaji msaada mkubwa zaidi katika maandalizi ya mechi za kiwango kikubwa kama hizi, hasa kuhusu uwanja wa nyumbani na mazingira ya haki kwa timu zote.
"Tunahitaji uungwaji mkono mkubwa zaidi kimazingira. Uwanja wa nyumbani ni sehemu ya ushindi. Tutajifunza, tutaamka, na tutarudi kwa nguvu kubwa zaidi," alisema kwa matumaini.
Simba sasa inageuza macho katika Ligi Kuu na nusu fainali ya Kombea FA na baada ha hapo maandalizi ya msimu ujao wa mashindano ya CAF, wakiwa na kiu ya kurejea tena fainali na kulipiza kisasi cha msimu huu.