Tshabalala: Tumepambana tatizo refa

Muktasari:
- Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi ya pili ya fainali dhidi ya RS Berkane, Tshabalala alisema wachezaji wa Simba walipambana kwa moyo wote, lakini walikumbwa na hali ambayo haikuwa sawa.
NAHODHA wa timu ya Simba, Mohammed Hussein 'Tshabalala', amesema licha ya juhudi kubwa walizoweka uwanjani kuhakikisha wanatwaa Kombe la Shirikisho Afrika, ndoto hiyo ilizimwa na maamuzi tata ya refa Dahane Beida kutoka Mauritania.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mechi ya pili ya fainali dhidi ya RS Berkane, Tshabalala alisema wachezaji wa Simba walipambana kwa moyo wote, lakini walikumbwa na hali ambayo haikuwa sawa.
"Tumepambana kuhakikisha kombe linabaki nyumbani, lakini imeshindikana. Kama wachezaji tumefanya kila jitihada, lakini kuna vitu ambavyo vimetokea na hatuwezi kuelewa," alisema kwa masikitiko.
Nahodha huyo ambaye pia ni beki wa kushoto wa Wekundu wa Msimbazi alisema, mechi hiyo ilikuwa mkononi mwao, lakini matukio ya kutiliwa shaka yaliwakatisha tamaa.
"Niwe mkweli, kila mtu ameona kilichotokea, sijui nisemeje. Ila kwa kweli mwamuzi ameiharibu fainali. Mechi tulikuwa tumeishika, tuliamini kuwa inawezekana kabisa kutwaa kombe. Lakini tukakumbwa na changamoto ya kadi, ikatufanya kuwa pungufu uwanjani na hali ikabadilika," aliongeza Tshabalala.
Katika mechi hiyo iliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, matokeo ambayo yaliwapa Wamorocco ubingwa kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-1.
Simba ilitangulia kupata bao kupitia kwa Joshua Mutale dakika ya 17, lakini RS Berkane ilisawazisha kipindi cha pili kupitia kwa Soumaila Sidibe, huku Simba ikimaliza mechi ikiwa pungufu baada ya Yusuph Kagoma kupewa kadi nyekundu dakika ya 50.
Tshabalala alihitimisha kwa kusema kuwa wanahitaji muda kupona kihisia, lakini watarejea wakiwa na nguvu zaidi msimu ujao.
"Tunawaomba radhi mashabiki wetu, tunajua waliamini sana. Hii ni sehemu ya mchezo, lakini kuna haja ya CAF kuangalia namna baadhi ya maamuzi yanavyofanyika katika mechi kubwa kama hizi," alisema.
Fainali hiyo imeacha mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka, huku wengi wakilalamikia maamuzi ya mwamuzi na matumizi ya teknolojia ya VAR.