C.I.N.T kuwanoa wasanii ukusanyaji ‘maokoto’ kwa wanaotumia kazi zao

wadau wakichangia mada

Muktasari:

  • Mtandao wa Tasnia Bunifu Tanzania (C.I.N.T), umeanza kuwajengea uwezo wasanii namna ya kuunda kampuni zao za  kukusanya mirabaha kwa niaba ya wanachama wao zinazoitwa Collective Management Oraganization(CMO).

Mtandao wa Tasnia Bunifu Tanzania(C.I.N.T), umeanza kuwajengea uwezo wasanii namna ya kuunda kampuni zao za  kukusanya mirabaha kwa niaba ya wanachama wao zinazoitwa Collective Management Oraganization(CMO).

Hivi karibuni kulifanyika mabadiliko madogo ya sharia ya hakimiliki na hakishiriki nchini iliyokuwa imeiunda Taasisi ya Hakimiliki na Hakishiriki (Cosota) ya  mwaka 1999.

Sheria hiyo ilikuwa ikiruhusu Cosota kusimamia hakimiliki nchini na wakati huohuo kugawa mirabaha kwa wasanii nchini.

Ni kutokana na mabadiliko hayo, sheria hiyo imewapa nguvu wasanii kukusanya mirabaha kwa niaba ya wanachama wao zikiitwaCMO’s.

Akizungumza katika warsha hiyo ya kuwajengea uwezo wasanii, Katibu Mkuu wa C.I.N.T, Innocent Nganyagwa’Ras Inno’, wameamua kuchukua jukumu hilo ili kutoa elimu watu wajiendae, kwa kuwa mfumo huo ni mpya watu wasije wakashtuka kama ilivyotokea kwenye mabadiliko ya sheria ya Hakimiliki na hakishiriki


“Kwa hiyo tunafanya warsha zipatazo tano tukiwa tunazungumzia mambo ya mirabaha , CMO’s lakini katika mawanda tofauti, hii ikiwa ni warsha yetu ya  pili kuifanya,”amesema Nganyagwa.

Amesema katika uundaji wa CMO’s hizo, mpaka sasa watu wa muziki ndio tayari wameshaunda yao huku watu wa filamu wakiwa mbioni kukamilisha ya kwao.

Wakizungumzia umuhimu wa warsha hiyo kwao, Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania, Adrian Nyangamale, amesema kukusanya hela kwa matumizi ya kazi zao ni eneo ambalo lilikuwa likilalamikiwa na wasanii tangu miaka 12 iliyopita.

“Hivyo kuletwa suala hilo kwa wadau ni jambo zuri na wanachokifanya C.I.N.T ni katika kutusaidia kuunda kampuni zilizo imara na kufanya kazi vile inavyotakiwa na kueleza hata wao wasanii Sanaa za maonyesho wapo katika mchakato wa kuanzisha yao.

Naye mchapishaji wa vitabu wa siku nyingi, Abdulllah Saiwaad, amesema tangu lilipotolewa tangazo Juni mwaka huu, wamekuwa wakijiandaaa.

Hata hivyo amesema moja ya changamoto inayowakabili katika kusajili kampuni zao ni masharti ya kutakiwa idadi kubwa ya wanachama wasiopungua 30, mchakato wa kupata leseni Brela na Mamlaka ya Mapato Tananzia(TRA) kuwa mrefu  na ndio maana tasnia nyingine za sanaa zimeonekana kuwa yuma kuanzisha CMO yao.

Dk Godwin Maimu maarufu ‘Dk Nnyaka’, kutoka katika tasnia ya Filamu, amesema elimu inayotolewa katika warsha hiyo ni kubwa na anaona  namna gani wasanii wanaweza kunufaika na kazi zao za ubunifu kwani ni muda mrefu zimekuwa zikitumiwa bila ya wao kunufaika.

‘Hata hivyo pamoja na Cosota kuwa na utaratibu wa kutoa mirabaha, Filamu hawajawahi kupata mgao, hivyo kwa ujio wa sheria hii sasa naona tunaenda kunufaika,niiombe jamii kuwa tayari kulipia,”amesema Dk Nyaka.