Bright- Huyu Miquissone ana balaa jamani

Muktasari:

  • Msanii  wa Bongo fleva, Said Rashid 'Bright' humwambii kitu kuhusiana  na winga wa Simba, Luis Miquissone  ambaye amemzungumzia kuwa  ameonyesha kiwango kisichokuwa na mpinzani kwenye Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa hivyo  ana uwezo wa kucheza  katika timu yoyote Afrika.

Msanii  wa Bongo fleva, Said Rashid 'Bright' humwambii kitu kuhusiana  na winga wa Simba, Luis Miquissone  ambaye amemzungumzia kuwa  ameonyesha kiwango kisichokuwa na mpinzani kwenye Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa hivyo  ana uwezo wa kucheza  katika timu yoyote Afrika.


Bright ambaye ni shabiki kindakindaki wa Simba amesema Miquissone ni mchezaji anayejipambanua ndani ya uwanja kujua afanye nini ili mradi timu yake inufaike hivyo ni ngumu kwa Simba kwa wakati huu kupoteza mchezo kizembe.  


Amesema hana maana kwamba Miquissone ndiye anafanya kazi peke yake, bali amekuwa akijiongeza pindi  anapoona timu inaelemewa na wakati mwingine kujitoa mhanga katikati ya mabeki, ili kwenda kufunga ama kusababisha faulo zenye faida kwa timu.
"Kwa ujumla kikosi cha Simba kipo imara na ndio maana kina ushindani wa wachezaji wanaoanza na wale ambao wanakaa benchi, lakini kila mmoja wao ana aina yake ya utendaji kazi, sawa na sisi kwenye muziki kila mmoja ana vionjo vyake vya namna ya kuifikia jamii tunayoipelekea kazi zetu," 


"Miquissone kuna wakati  analindwa na mabeki wengi wa timu pinzani  lakini bado anawafuata bila kujali kuumia.Anaonyesha jinsi ambavyo anataka kujitofautisha na wengine,"amesema Bright.


Amesema ana matumaini kwa aina ya uchezaji wake, timu zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa na ligi ya ndani zinatamani kuwa na mchezaji wa aina yake ambaye muda wote anakuwa anawapa mawazo mabeki jinsi ya kumkaba.