Bodi ya ligi yafungia Uwanja wa Mabatini

Saturday January 15 2022
mabatini pic
By Daudi Elibahati

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeufungia uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani kuendelea kutumika kwa michezo ya Ligi hadi hapo utakapofanyiwa marekebisho kwenye eneo la kuchezea.

Taarifa iliyotolewa na TPLB imeeleza kuwa eneo la kuchezea la uwanja huo linatakiwa kusawazishwa vizuri na majani yake kustawishwa vema ili uweze kuendana na matakwa ya kikanuni na sheria namba moja ya mpira wa miguu inayozungumzia uwanja.

Kufuatia taarifa hiyo, klabu ya Ruvu Shooting ambayo ilikuwa ikiutumia kama uwanja wake wa nyumbani italazimika kuhamia uwanja wa Uhuru uliopo Jijini Dar es Salaam.

Kamati ya leseni za klabu itaukagua uwanja huo mara baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo ili kujiridhisha kuwa unafaa kuendelea kutumika kwa michezo ya ligi.

Bodi inaendelea kuzikumbusha klabu zote kuhakikisha viwanja vyao vya nyumbani vinakuwa katika hali nzuri wakati wote kwani viwanja ambavyo vitakosa sifa vitafungiwa mara moja.

Advertisement