Bocco Simba mdogomdogo

Moto mpya Yanga ni noma

KOCHA wa Simba, Didier Gomes amesema nahodha wa timu hiyo, John Bocco ameanza kumpa dakika chache za kucheza dhidi ya African Lyon mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam, lengo ni kumrejesha mdogomdogo mchezoni.

Tangu Bocco alipoumia baada ya mechi yao na FC Platinum ya Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya kuitwa Taifa Stars iliyokuwa imekwenda Cameroon kwenye fainali ya Chan, hakuonekana uwanjani, ingawa alikuwa anakaa benchi baadhi ya mechi.

Katika mechi hiyo, Gomes alimwingiza Bocco dakika ya 81 kubadili nafasi ya Meddie Kagere na mara baada ya mechi, alisema atakuwa anaendelea kumwongezea dakika za kucheza kwa kadri atakavyokuwa fiti.

“Natambua Bocco ni mchezaji mzuri sana, lakini siwezi kuanza kumpa dakika nyingi kwani bado hajawa fiti asilimia 100, ndio maana nitaanza na dakika 15, atakuja 20 na kisha kucheza gemu nzima kulingana na maendeleo yake ambayo atakuwa anayaonyesha,” alisema Gomes na aliongeza;

“Pamoja na hilo anaendelea vizuri tofauti na mwanzo na nilikuwa siwezi kumpa mechi za kucheza, baada ya siku kadha atarejea kwenye makali yake, kwani ni mchezaji muhimu na anayejituma kwa nafasi yake.”

Alisema kwa rekodi za Bocco anajua fika ni mchezaji mpambanaji anayejua kufunga hilo analitarajia kuliona wakati wowote kwake na yupo karibu naye kuona anakaa sawa kisaikolojia muda ambao anapigania kukaa sawa. Strika huyo anashika nafasi ya pili Ligi Kuu akiwa na mabao nane nyuma ya Meddie Kagere mwenye mabao tisa.

Mbali na hilo alizungumzia mchezo wao na Lyon aliotumia baadhi ya wachezaji waliokuwa hawaanzi kikosi cha kwanza, wameonyesha picha ya nini cha kufanya zaidi kwenye mechi zilizopo mbele yao.

“Ni wachezaji wazuri ambao watafanya kazi nzuri kulingana na majukumu yaliopo mbele yetu, bila shaka naamini wataipambania timu kulingana na uwezo wao,” alisema.