Prime
Nondo za Lejendi... Tatizo liko hapa, marefa mnawaonea tu!

Muktasari:
- Nikaja kugundua kwamba ina maana hata mwamuzi anasubiria simu za viongozi wa timu zinazocheza mechi na mwenye kisu kikali atakula nyama.
NITAANZA kwa kukupa mfano mmoja. Nimewahi kwenda sehemu sitapataja moja kwa moja. Ilikuwa ni ngazi ya wilaya. Nilishuhudia baada ya kumalizika kikao cha mechi wasimamizi wanamuuliza kiongozi wa timu unahitaji namba ya mwamuzi? Nilishtuka, lakini nikaendelea kutega sikio nielewe ni nini hasa kinaendelea.
Nikaja kugundua kwamba ina maana hata mwamuzi anasubiria simu za viongozi wa timu zinazocheza mechi na mwenye kisu kikali atakula nyama. Ndio Afrika ilipofikia, haya mambo ukizungumza yanaweza kuonekana ya ajabu sana, lakini chini haya mambo yapo na ndio yanaendelea hadi kuja kutengeneza hili tatizo kubwa lililoko katika ligi za juu.
Huko ni ngazi za chini, sasa tatizo la waamuzi kuzisaidia baadhi ya timu hususani hawa mapacha wa Kariakoo ni mbegu ambayo imepandwa kuanzia ngazi za awali na bahati mbaya zinapandwa na viongozi wanaowakuta katika soka wakati wanaanza safari yao.
Hapo uzoefu wangu unaonyesha huwa iko hivi; ikitokea timu inaonekana inajiweza kiuchumi na ikawa kimya uwezekano wa kufanyiwa figisu upo. Kuna namna ambayo huku kwenye Ligi za Wilaya waamuzi wanahisi ni wajibu wa klabu kununua haki au kulipia upendeleo.
Mimi siwaoni waamuzi kama tatizo bali tatizo ni mfumo kuanzia wanaowasimamia waamuzi, viongozi wa klabu na waamuzi kama wahusika wakuu.
Kuna mashindano wameshachoka kulalamika kila mmoja anamdhulumu mnyonge wake mfano mzuri ni Championship timu haipandi kwa kuwa tuu na kikosi bora na benchi la ufundi inapaswa kuwa na bajeti ya kununua haki au upendeleo katika maeneo mengi ni hili ukienda viwanjani ukafanya utafiti kama wa kwangu utaelewa.
Tukirudi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambako kunapigiwa kelele sababu ndicho kioo cha mpira wetu timu zote zinafaidika kwa nyakati tofauti japo Simba na Yanga ni wanufaika wakuu kwenye maeneo tofauti.
Simba na Yanga kutokana na kuwa na ufuasi mkubwa wamejikuta wakifaidika na maamuzi mengi ya kuwasaidia ndani ya uwanja sababu asilimia kubwa ya waamuzi ni wapenzi na mashabiki wa timu hizo hivyo mbali na vishawishi vingine pia husukumwa na mapenzi.
Hiyo ni kama ambavyo klabu hizi zinapambana kuhakikisha zinaweka wapenzi na mashabiki wao katika ngazi mbalimbali za maamuzi kwenye soka ndivyo wanavyopambana kuwaingiza waamuzi wenye vinasaba nao kwenye mfumo ili waje kuwapambania mbio za kuwania mataji.
Ili kukabiliana na changamoto hii tunahitaji uadilifu na sio kubadilisha sura na majina ya watendaji. Uadilifu ukianzia ngazi za juu na kuacha kupigania maslahi ya klabu bali maslahi ya mchezo wenyewe tunaweza kuondoa changamoto hizi za usimamizi wa kanuni na sheria tulizojiwekea.
Yaandaliwe mazingira rafiki ya kazi kwa waamuzi na kuwaondoa kwenye makucha ya klabu kwa kuwawezesha kiuchumi na kuwafanya waweze kufika kwenye vituo vyao vya kazi bila fadhila za klabu.
Kuboresha adhabu zilizopo badala ya kuwatoa mizunguko miwili au mitatu waondolewe kwenye ratiba kwa yale makosa yakawaida au kuwashusha daraja ili kuendelea kuwafuatilia kwa yale makosa makubwa wafutwe kabisa ili kuusafisha mchezo na kubaki na wachache wenye uwezo ambao watajenga hadhi na thamani ya tasnia ya waamuzi kwa kuweka usawa wa timu kushindana.
Tukifanikiwa kuwa na nafasi sawa ya kupata ushindi mbele ya sheria tutaongeza matamanio kwa klabu kujiimarisha kwa kusajili kikosi bora na kuwa na mabenchi imara hivyo kuongeza ushindani na kufanya tuwe na Ligi bora ambayo aliyejiandaa vizuri ashinde na kupata bingwa na wawakilishi wanastahili na hata wanaoshuka daraja wajue ni kwa sababu wameshindwa ki mbinu na ufundi ndani ya kiwanja kuliko ilivyo sasa.
Unapoandaa bajeti ya timu uandae na bajeti ya kununua haki kwa namna mbalimbali na wakati mwingine kupanda au kushuka haitegemei ubora wa timu pekee.
Katika hili wenye mamlaka wakiamua tunaweza kupiga vita rushwa na upangaji matokeo kwenye ligi zetu.
Mimi naamini kama kutakua na haki katika kushindana hata hizi alama zinazokusanywa na timu bingwa zinaweza zisifikiwe ni kila aliekabidhiwa nafasi ya uongozi kwenye mihimili yetu ya soka avue jezi ya timu yake ya Kariakoo na avae jezi ya taifa.