Prime
Mahakama yafanya uamuzi kesi Dabi ya Kariakoo

Muktasari:
- Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Simba ambao awali ulipangwa kupigwa Machi 8, mwaka huu, uliahirishwa na Bodi ya Ligi (TPLB), baada ya Simba kulalamika kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, suala ambalo liliughafilisha upande wa Yanga ambao umegomea ratiba ya pili iliyopangwa kwamba mechi ichezwe Juni 15.
SAKATA la mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambalo Yanga imeapa kuwa haitapeleka timu uwanjani Juni 15, mwaka huu, limechukua sura mpya baada ya kuwasilishwa mahakamani na mmoja wa wanachama wa Yanga, ambako hata hivyo chombo hicho cha kutafsiri sheria kimetoa uamuzi rasmi leo, Ijumaa, Juni 6, 2025.
Mchezo huo wa Yanga dhidi ya Simba ambao awali ulipangwa kupigwa Machi 8, mwaka huu, uliahirishwa na Bodi ya Ligi (TPLB), baada ya Simba kulalamika kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, suala ambalo liliughafilisha upande wa Yanga ambao umegomea ratiba ya pili iliyopangwa kwamba mechi ichezwe Juni 15.
Lakini, leo, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imejiweka pembeni katika kesi ya kuzuia mechi hiyo ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba maarufu kama Dabi ya Kariakoo iliyopangwa kuchezwa Juni 15, 2025, baada ya kuamua kuwa haina mamlaka ya kuisikiliza.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mwanachama wa Yanga kutoka Iringa, Dk Samweli Marwa Chacha dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na Bodi ya Ligi (TPLB) pamoja akiomba kufutwa kwa ratiba mpya ya mechi hiyo na Yanga ipewe alama tatu.
Hata hivyo, TFF na TPLB kupitia wakili Rahim Shaban iliweka pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo ikidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa leo, Ijumaa na Jaji Elizabeth Mkwizu aliyesikiliza pingamizi hilo imekubaliana na hoja za pingamizi la TFF na TPLB, na kutupilia mbali kesi hiyo.
Jaji Mkwizu amesema kuwa Katiba ya TFF na ya Yanga ambayo mdai ni mwanachama inazuia wanachama kupeleka masuala ya migogoro ya uendeshaji wa mchezo huo katika mahakama za kisheria, bali masuala hayo yanaweza kushughulikiwa na vyombo vya ndani ya TFF au Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).
"Kwa kuzingatia hoja hizo mahakama hii inakosa mamlaka ya kusikiliza shauri hili, hivyo shauri linatupiliwa mbali," amesema Jaji Mkwizu.
Juzi wanachama wa Yanga kwenye mkutano jijini Dar es Salaam walisisitiza kwa kusema ‘HATUCHEZI’ huku wakitoa hoja mpya kwa mabosi wa klabu hiyo kama watakiuka msimamo huo, basi wajue mlango wa kutokea utakuwa wazi.
Mkutano huo uliofanyika katika makao ya klabu hiyo Jangwani, wanachama hao wa matawi wakijumuishwa wazee walitoa msimamo mkali kwa uongozi kuhusiana na mechi hiyo wakisema timu hiyo haitakwenda uwanjani hadi mambo ya msingi yafanyiwe kazi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mohammed Msumi hadi inapangwa tarehe ya mechi hiyo inayotakiwa kupigwa Juni 15, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) waliotoa sababu za msingi zilizosababisha mechi ya Machi 8 kuahirishwa.
Mratibu wa matawi ya Yanga, Shaaban Mgonja alienda mbali akisema mkutano wa matawi umekubaliana kwamba, hakutakuwa na mchezo huo na endapo kiongozi yeyote atakwenda kinyume na msimamo huo anaruhusiwa kupisha klabuni hapo kwa kuondoka.
Kwa mujibu wa kanuni ya ligi, timu isiyofika uwanjani kwa mechi moja inapoteza pointi tatu na mabao matatu, lakini itakatwa pointi 15 katika zile ilizonazo, jambo ambalo Yanga imekuwa ikisisitiza ipo tayari ilimradi, kwa maelezo Bodi ilishindwa kusimamia kanuni hizo za ligi katika mechi ya Machi 8.
Hilo ni pambano la 114 kwa watani wa jadi kama watakutana Juni 15 katika mechi za ligi tangu 1965 na la pili msimu huu, kwani la kwanza Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa dakika ya 86 na beki wa Simba, Kelvin Kijiri aliyejifunga wakati akiokoa shambulizi lililotokana na mpira wa Maxi Nzengeli.