Beki wa Simba, Bukungu atua kwa kishindo KMC

Muktasari:
KMC inajiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Kagame
Dar es Salaam. Beki wa zamani wa Simba kutoka DR Congo, Janvier Besala Bukungu amejiunga na KMC kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta ameiambia MCL Digital kwamba Bukungu amejiunga na klabu hiyo kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kuelekea katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Kombe la Kagame na Ligi Kuu Bara.
Alisema mchezaji huyu anaungana na nyota wengine tisa waliosajiliwa katika kikosi chetu kwa ajili ya kujianda na msimu ujao.
Usajili wa Bukungu unamrudisha kwa mara nyingine nchini kucheza soka akiwa chini ya kocha wake Jackson Mayanja waliowafanya kazi pamoja Simba msimu wa 2016-17.
Mbali na Bukungu, Sitta alisema wako mbioni kunasa saini ya kiungo mshambuliaji kutoka Togo, lakini hakutaka kuweka wazi jina lake.
"Tutakapokamilisha usajili wake, tutamuweka wazi, lakini kila kitu kinakwenda vizuri na huyo ndiye mchezaji wa mwisho kusajiliwa kwenye kikosi chetu kipindi hiki kwani tunafunga zoezi la usajili," alisema Sitta.