Azam yapiga mkwara mapema

Thursday July 22 2021
azam pic
By Thomas Ng'itu

USAJILI unaofanywa na mabosi wa Azam FC unaonyesha kabisa wanataka kuongeza ushindani zaidi msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, baada ya kubaini kwamba kuna sehemu walikosea misimu iliiyopita na kukosa ubingwa wa ligi.

Hiyo ni baada ya kuendelea kuweka wazi usajili ambao hadi sasa wamewashusha nyota Charles Zulu, Rodgers Kolla na Edward Manyama huku wakiwaongezea mikataba wachezaji wengine Ayoub Lyanga, Prince Dube na Bryson Rafael.

Ofisa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alisema usajili wanaofanya ni kwa ajili ya kuleta ushindani msimu ujao na mashindano watakayoshiriki ikiwemo kimataifa.

“Tunataka kuwa na ushindani msimu ujao na ndio maana tunafanya usajili, bado wachezaji wawili kuwasajili, kiungo mkabaji na mchezeshaji ambao muda wowote watasaini, kwa ndani hatutosaini mchezaji ambaye hayupo kwenye mipango ya kocha,” alisema Popat.

Alisema kwasasa timu ipo mapumziko ya wiki tatu, lakini wakirejea wataenda kuweka kambi nje ya nchi ili kupata mechi za kirafiki zitakazowajenga kwenye maandalizi ya msimu ujao.

“Wachezaji wapo mapumziko, baada ya hapo watarudi kambini na kuendeleza programu ya kocha kwa siku saba hadi nane, tutaenda kuweka kambi nchi za jirani.”

Advertisement

Azam imemaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu na kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao. Ufanisi wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa msimu uliopita umeiongezea Tanzania nafasi ambazo Azam, Biashara ni wafaidika.

Advertisement