Azam FC: Tuleteeni hao Simba

Unguja. Waleteni na hao! Ndivyo wanavyokuambia  Azam FC baada ya kuondosha Yanga kwa mikwaju ya penalti 9-8 ikiwa ni mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi inayofanyika Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Katika dakika 90 za mchezo huo timu hizo zilitoka bila kufungana hivyo kulazimisha kupigwa mikwaju hiyo ambapo Yassin Mustafa ndiye aliyepeleka kilio kwa wanajangwani hao baada ya kukosa penati ya nane.

Upande wa Yanga waliopata penalti hizo ni Jesus Moloko, Zawadi Mauya, Dickson Job, Fiston Mayele, Saido Ntibazonkiza, Yannick Bangala, Dickson Ambundo na Farid Mussa

Upande wa Azam penalti zilipigwa na Lusajo Mwaikenda, Rodgers Kola, Kenneth Muguna, Yahaya Zayd, Agrey Morris, Daniel Amouh, Tepsi  Evance, Paul Katema na Mudathir Yahya.

Kwa matokeo hayo Azam atamsubiri mshindi kati ya Simba na Namungo Fc ambao mechi yao itaanza saa 2.15 usiku wa leo Jumatatu huku fainali hizo zikitarajiwa kuchezwa Januari 13 mwaka huu.

Kocha wa Azam Fc Mohamed amesema aliwaandaa wachezaji wake kisaikolojia na kwamba wanakwenda kukutana na timu bora ambayo iliwafunga kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

"Ukicheza mechi kama hizi ambazo zinawalazimu kuingia hatua ya matuta kama kutakuwa na sare lazima ujiandar kwa hilo hivyo nilijiandaa kwa kitu kama hicho na sasa namsubiri mpinzani wangu awe Simba ama Namungo tupo tayari," amesema Mohammed

Katika mechi za ligi kuu Bara Simba iliifunga Azam bao 2-0 huku Azam nayo ikipata ushindi kwa Namungo na hata walipokutana kwenye mechi ya makundi ya Kombe la Mapinduzi Azam iliifunga Namungo bao 1-0.

Kwa upande wa kocha wa Yanga Cedric Kaze amewapongeza Azam kwa mchezo mzuri na kukiri kwamba kikosi chake kuna wakati kilipotea.

"Tumeshindwa kutetea ubingwa na niliwaandaa pia wachezaji katika upigaji penalti lakini matokeo yamekuwa tofauti," amesema Kaze