Ambundo suala la muda Mbeya City

Muktasari:
- Nyota huyo pia amewahi kuzitumikia Dodoma Jiji, Alliance na Yanga na Singida Big Stars, alikuwa Fountain Gate kwa misimu miwili kabla ya miezi kadhaa iliyopita kuripotiwa kuondoka kambini.
INAELEZWA kwamba hesabu za Mbeya City sasa ziko kwa Dickson Ambundo, nyota mwenye uwezo wa kucheza kiungo mshambuliaji ambapo msimu wa 2024-2025 aliitumikia Fountain Gate.
Nyota huyo pia amewahi kuzitumikia Dodoma Jiji, Alliance na Yanga na Singida Big Stars, alikuwa Fountain Gate kwa misimu miwili kabla ya miezi kadhaa iliyopita kuripotiwa kuondoka kambini.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa: “Mbeya City iko katika hatua za mwisho kumchukua mchezaji huyo ili kuongeza nguvu kuelekea msimu ujao.”
Mwanaspoti lilipomsaka Ambundo, alisema: “Kwa sasa mimi ni mchezaji huru, kuwa na ofa hasa mwisho wa msimu ni jambo la kawaida tu, hivyo muda ukifika itajulikana.”
Mbeya City itashiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kukosekana kwa misimu miwili kwani ilishuka daraja msimu wa 2022-2023. Mbali na Mbeya City, timu nyingine iliyopanda ni Mtibwa Sugar ambayo nayo ilishuka msimu wa 2023-2024.