Al Ahly kuibomoa Simba kwa Miquissone

Thursday July 22 2021
luis pic
By Charles Abel

Mabingwa wa Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly wako katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa winga wa Simba, Luis Miquissone katika dirisha hili la usajili

Taarifa za mitandao ya Kingfut na El-Ahly ya Misri zimefichua kuwa uongozi wa Al Ahly umefikia makubaliano na Simba juu ya uhamisho wa nyota huyo raia wa Msumbiji

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Simba imeridhia kumuuza Miquissone kwa Al Ahly baada ya klabu hiyo ya Misri kuwasilisha rasmi ofa ya kumhitaji winga huyo.

Mara baada ya mazungumzo hayo kukamilika na klabu hizo kukubaliana, taarifa hizo zinafichua kuwa Simba imewapa ruhusa Al Ahly kumalizana na Miquissone kwenye suala la maslahi binafsi kabla ya kukamilisha rasmi mchakato wa usajili huo.

Usajili wa Miquissone umetokana na mapendekezo ya benchi la ufundi la Al Ahly chini ya Kocha Pitso Mosimane ambaye aliwahi kumnoa winga huyo pindi alipokuwa katika timu ya Mamelodi ya Afrika Kusini.

Kabla na hata baada ya Simba kukutana na Al Ahly, Mosimane alionyesha kukoshwa na kiwango cha Miquissone na kumtaja kama mmoja wa wachezaji mahiri na bora katika kikosi cha Simba.

Advertisement

”Ninamtambua Luis ni moja kati ya wachezaji wazuri, hata kabla ya mchezo wetu niliwaambia wachezaji wangu kwamba wanakutana na wachezaji wenye uwezo mkubwa ndani ya uwanja ikiwa ni pamoja na Luis.

Ninapenda kuona kazi yake ndani ya uwanja na ni moja kati ya wachezaji ambao walitupa changamoto kubwa katika mchezo wetu," alinukuliwa Mosimane mara baada ya mchezo ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly wa hatua ya makundi uliochezwa Februari, 23 mwaka huu ambao Miquissone alifunga bao hilo pekee.
Advertisement