Ajibu achimba mkwara Ligi Kuu

Muktasari:
- Ajibu amejiunga na Dodoma Jiji FC akitokea Coastal Union yenye maskani yake jijini Tanga. Pia amewahi kucheza klabu kadhaa hapa nchini zikiwemo Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars.
KIUNGO Mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Ibrahim Ajibu ameweka wazi kwamba anaamini msimu ujao wa 2024/25 timu hiyo itakuwa ndani ya Ligi Kuu Bara kutokana na usajili bora uliofanyika.
Ajibu amejiunga na Dodoma Jiji FC akitokea Coastal Union yenye maskani yake jijini Tanga. Pia amewahi kucheza klabu kadhaa hapa nchini zikiwemo Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ajibu amesema anaamini miongoni mwa timu ambazo zitakuwa tishio msimu ujao katika Ligi Kuu Bara ni pamoja na Dodoma Jiji FC kwa namna ambavyo wamesajili nyota wengi wenye viwango vikubwa.
“Usajili umefanywa vizuri na viongozi kwa hiyo tusubiri mashindano yaanze lakini matumaini ya kufanya vyema ni makubwa sana,” alisema Ajibu.
Akizungumzia mikakati yake kama mchezaji, Ajibu amesema anaendelea na mazoezi kwa kushirikiana na wenzake ili Ligi ikianza aweze kufanya kweli na kuisadia timu kumaliza katika nafasi za juu.
Nyota huyo ambaye amewahi kuitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kwa nyakati tofauti amelipongeza pia benchi la ufundi la timu yake linaloongozwa na Kocha Mkuu, Mecky Maxime.
“Benchi la ufundi kwa ujumla lote liko vizuri, hakuna changamoto yoyote nadhani watatusimamia vizuri na tutafika malengo ambayo tumejiwekea," alisema Ajibu.