Yanga yapewa mwamuzi wa bahati

YANGA iko jijini Pretoria Afrika Kusini kusaka tiketi ya kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati itakapocheza na Mamelodi Sundowns katika mchezo wa hatua ya robo fainali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld.
Mchezo huo wa marudiano utakaopigwa kesho umepangiwa kuchezeshwa na mwamuzi wa kati, Dahane Beida kutoka Mauritania huku akiwa na bahati nzuri na wawakilishi hao wa Tanzania kwani kabla ya hapo aliwahi kuichezesha na kupata ushindi mzuri, lakini pia ndiye aliyekuwa kwenye chumba cha VAR katika mechi ya Simba ya Ijumaa iliyopita ambayo Wekundu wa Msimbazi walilala 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikihitaji ushindi au sare yoyote ya mabao ili kutinga hatua ya nusu fainali baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Machi 30 mwaka huu kuisha kwa suluhu.
Rekodi zinaonyesha mwamuzi huyo amechezesha michezo 16 ya kimataifa ambapo timu mwenyeji imeshinda minane, sare minne na kupoteza minne huku katika mechi hizo, Dahane ametoa jumla ya kadi za njano 78 na kwa upande wa nyekundu ametoa mbili.
Mwamuzi huyo pia anakumbukwa kwani alichezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita wakati Yanga iliposhinda bao 1-0 dhidi ya USM Alger katika mechi ya marudiano iliyopigwa jijini Algeria Juni 3, mwaka jana.
Ushindi huo uliinyima Yanga ubingwa wa kombe hilo msimu uliopita kutokana na kanuni ya mabao mengi ya ugenini kwani ilishindwa kutamba katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ambayo ilifungwa 2-1, Mei 28 mwaka jana.
Dahane amewahi kuchezesha mchezo wa michuano ya Kombe la African Football League (AFL) hatua ya robo fainali kati ya Simba na Al Ahly ya Misri, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Oktoba 20, mwaka jana na kumalizika kwa sare ya 2-2.
Yanga ilifika hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye kundi 'D' na pointi nane nyuma ya Al Ahly iliyomaliza na pointi 12.