Try Again: Burudani ipo Simba mjiandae

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kuwaambia wajitokeze kwa wingi kwenye Simba Day kwani burudani ndio ipo huko kwani watashuhudia mashine zao za msimu wa 2022-2023.

Licha ya kuishuhudia timu hiyo ikiwa kambini jijini Ismailia, Misri kabla ya jana kurejea, mashabiki wa Simba wamekuwa kama wameingiwa ubaridi kwa usajili uliofanywa, lakini Try Again aliwahakikishia kwamba burudani wataipata Kwa Mkapa kwenye Simba Day.

Simba imewasajili Moses Phiri, Nassoro Kapama, Habib Kyombo, Mohammed Quattara, Augustine Okra, Nelson Okwa na Victor Akpan.

Akizungumza na Mwanaspoti Try Again alisema, wamefanya usajili mzuri ambao utakuwa na tija na manufaa na timu hiyo ili kurejesha heshima ya miaka minne mfululizo na kwamba salamu zitaanza mapema kwenye Simba Day inayofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumatatu ijayo.

Try Again alisema, msimu uliopita 2021/22 walipoteza mataji kitendo ambacho hakuna mwanasimba aliyekifurahia, hivyo wamejitahidi kuboresha maeneo ambayo yanahitajika kuboreshwa na msimu ujao moto utawaka kwelikweli kurejesha heshima yao.

“Wanasimba wasijali Simba imefanya usajili mzuri na mkubwa sana, kila mchezaji aliyesajiliwa anahitajika kikosini, hivyo basi nawaomba wakae mkao wa kula wataujua usajili wao wote,”

“Tunafanya sajili zetu kwa kufuata matakwa ya kocha, na ndio maana tumeboresha kila sehemu kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji husika,” alisema Try Again aliyewahimiza mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha la Simba Day litakalosindikizwa na mechi ya kirafiki ya kimataifa ambapo licha ya kufanywa siri, lakini inadaiwa timu ya St George ya Ethiopia huenda ndio itakayocheza mechi hiyo.