Simba, Yanga zote nd'o kama hivyo

Simba, Yanga zote nd'o kama hivyo

TIMU ya Ihefu iliyopo mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ni kama imepata ahueni baada ya Bodi ya Ligi (TPLB) kuahirisha mchezo wao na Yanga uliokuwa upigwe wiki ijayo na kupelekwa hadi Novemba 29, huku mechi za timu za taifa zikitajwa ndio sababu na kuahirishwa mechi hizo na nyingine tano.

Ihefu ilikuwa iialike Yanga Septemba 29, siku moja baada ya Simba kucheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya mechi iliyoangwa sasa kupigwa Novemva 23.

Bodi ya Ligi ilitangaza jana kuahirishwa kwa mechi hizo za vigogo na nyingine nne, huku taarifa hiyo ikionekana ni nafuu ya Ihefu iliyopoteza mechi nne mfululizo na kuburuza mkia.

Japo bodi haikuanisha sababu za mechi hizo kuahirishwa, lakini habari za uhakika ilizonazo Mwanaspoti ni kwamba michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa za Taifa Stars nchini Libya na zile za U23 inayowania fainali za Afcon ndio chanzo.

Stars itacheza kirafiki Septemba 24 na Uganda kisha Septemba 27 itamalizana na Libya zikiwa ni mechi za maandaliziya kusaka tiketi za Afcon 2023, Tanzania ikiwa Kundi F na Uganda, Algeria na Niger.

Yanga ina wachezaji watatu Stars ambao ni Kibwana Shomari, Dickson Job na Feisal Salum, wakati Simba ina Aishi Manula, Beno Kakolanya, Mzamiru Yassin na Habib Kyombo wakati Azam yupo Sospeter Bajana. Pia beki Henock Inonga wa Simba na kipa Diarra Djigui wa Yanga wameitwa timu za taifa za DR Congo na Mali.

Kwa upande wa U23, Yanga ina; kipa Abuutwalib Mshery, David Brayson na Denis Nkane, huku Simba ikiwa haina yeyote na Azam imetoa Zubery Masoud, Nathaniel Chilambo, Pascal Msindo, Twalib Mohamed, Tepsie Evance na Abdul Suleiman ‘Sopu’.

Mechi nyingine zilizobadilishwa ni kati ya KMC na Mtibwa iliyokuwa ipigwe Septemba 27 sasa itachezwa Oktoba 15, ile ya Ruvu Shooting na Coastal Union ilikuwa ipigwe Septemba 26 sasa itachezwa Septemba 29, Polisi Tanzania na Namungo imesogezwa Oktoba 19 kutoka Septemba 27 na ile ya Kagera Sugar na Singida Big Stars imepangwa kupigwa Oktoba 21 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba badala kupigwa Septemba 28 Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza,