Simba kubeba kipa wa Yanga

SIKU chache baada ya Yanga kutangaza kusaka kipa mpya, mabosi wa Simba nao wamejiongeza kumnasa kipa wa kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jeremiah Kisubi aliyeomba apekwe kwa mkopo Tanzania Prisons.

Awali ilielezwa Simba haikuwa na mpango wa kipa mpya kwani tayari kikosini inao Aishi Manula, Beno Kakolanya, Kisubi na Ally Salum, lakini kuondoka kwa Kisubi, huku Manula akikosa mtu wa kumpa ushindani, imewalazimu mabosi hao kusaka kipa huyo mpya.

Hesabu zao za haraka zimeenda kwa kipa wa zamani wa Yanga, Metacha Mnata aliyewekwa kundi la nyota wapya wanaotakiwa Msimbazi akiwemo winga Harrison Mwendwa na straika Alex Bazo anayecheza Nkana ya Zambia.

Mwanaspoti linafahamu kamati hiyo ya usajili Simba imefanya maamuzi magumu ya kumfuata Metacha anayecheza Polisi Tanzania, ikionyesha kumuamini anaweza kumpa presha Manula anayechuana naye pia Taifa Stars.

Tayari Simba imeenda kuzungumza na viongozi wa Polisi ili Metacha atue Msimbazi, licha ya kuwa na mkataba aliosaini alipotemwa na Yanga.

Hata hivyo, inaelezwa Simba imeambiwa ili kumpata Metacha inatakiwa kulipa kiasi cha pesa kwenye mkataba wake uliosaliwa wa mwaka mmoja na nusu kisha imalizane naye kimasilahi.

Meneja wa Metacha, Jemedari Kazumari alisema ni kweli Yanga ilikuwa ya kwanza kumfuta kisha ikafuata Simba.

“Kiongozi mmoja wa juu Yanga mwenye sauti aliwafuata mabosi wa Polisi kuona jinsi ya kumpata Metacha baada ya hapo walipewa majibu na wamekwenda kujipanga,” alisema Jemedari na kuongeza;

“Suala hilo la Simba nao wanatakiwa kufuata utaratibu kwani Metacha bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu na Polisi.”

Metacha alipotafutwa alisema; “Timu yoyote wanaonihitaji wanatakiwa kufanya mambo mawili kuwasiliana na uongozi wa Polisi na upande wangu.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania, Robert Munisi alisema wanalisikia Metacha kuhitajika Simba na Yanga, ila hakuna taarifa rasmi. “Katika meza yetu si Simba wala Yanga walioleta ombi la kumtaka kipa wetu.”