Simba inaanza na staa huyu

Simba inaanza na staa huyu

MABOSI wa Simba wapo sokoni kutafuta nyota wapya watakaowasajili dirisha la usajili litakapofunguliwa ili kuongeza makali ya kikosi hicho msimu ujao kutimiza lengo lao la kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Eneo waliloanza nalo ni ushambuliaji wa kati kutokana na John Bocco, Meddie Kagere na Chriss Mugalu kushindwa kuonyesha cheche zao kama ilivyotarajiwa msimu huu.

Mabosi hao wa Simba wametua kwa Mkongomani anayeichezea timu ya Taifa ya Afrika ya Kati, Ceasar Lobi Manzoki ambaye ni mfungaji anayeongoza kwenye Ligi Kuu ya Uganda akiwa na mabao 18. Anaichezea Vipers ya Uganda ambayo tayari ni mabingwa wa Ligi Kuu ya nchini humo inayomalizika wikiendi hii.

Staa huyo mwenye urefu sawa na Meddie Kagere ametupia mabao hayo 18 kwenye mechi 29 na leo atakosa mchezo wa kufunga msimu kutokana na kupata majeraha ya kichwa kwenye mchezo uliopita. Msimu uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwake Uganda alifunga mabao saba.

Taarifa kutoka ndani ya Simba ni kwamba uongozi wa timu hiyo ulimtuma kigogo wao mmoja kwenda Uganda kumuangalia Manzoki anavyocheza na uwezo wake wa kufunga mabao kama anaweza kufiti ndani ya kikosi chao.

Simba imejiridhisha kwamba staa huyo aina yake ya uchezaji inataka kufanana na Kagere na hawana tofauti kubwa ingawa Simba wanaamini kuwa wachezaji waotokea ukanda unaoongea lugha ya Kifaransa wana juhudi kubwa kuliko wale wa Afrika Mashariki.

Habari zinasema kwamba Simba katika nyakati tofauti imewasiliana na Manzoki na kuzungumza juu ya suala la kumsainisha mkataba na wameshakubaliana mambo kadhaa ingawa wao kwa wao ndani kuna baadhi wana wasiwasi na kiwango cha staa huyo.

Waliovutiwa na mchezaji huyo wanamuelezea kama mtu mwenye uwezo wa kufunga mabao, kuwasumbua mabeki wa timu pinzani kutokana na umachachari wake.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipoulizwa kuhusiana na usajili mpya, alisema kocha wao Pablo Franco ndio mwenye uamuzi kuhusiana na suala lolote la kiufundi.

Kwa upande wa Manzoki alisema kuna klabu tatu kutoka Tanzania amefanya nazo mawasiliano na kuonyesha nia ya kumuhitaji ila hadi wakati huu hajafanya uamuzi ya kwenda kusaini.

“Siwezi kuziweka wazi klabu hizo ila ni kweli kuna moja ambayo hadi masuala ya kimaslahi tumezungumza ila bado hatujafikia kwenye eneo la uamuzi ili kuja huko kujiunga nayo,” alisema Manzoki.

Kwa mujibu wa mitandao, Manzoki alizaliwa Oktoba 12, 1996 DR Congo, ni raia wa nchi hiyo ambayo ameitumikia timu ya taifa hilo katika mechi tatu mwaka 2016, kabla ya kufanya uamuzi wa kuchukua uraia wa Afrika ya Kati 2022.

Vipers ilimsajili Manzoki kwa mkataba wa miaka miwili akitokea AS Vita ya DR Congo na mwisho wa msimu huu atakuwa mchezaji huru na hadi sasa bado hajasaini mkataba mpya wa kusalia klabuni hapo.

Mastraika wa Simba, Bocco na Mugalu walimaliza wafungaji bora Na 1 na Na2 msimu uliopita, lakini msimu huu wameanza kwa kusuasua.