Prisons yarudi rasmi Rukwa

Wednesday October 13 2021
PRISON PIC
By Saddam Sadick

Mbeya. Baada ya kumaliza mechi yake ya kirafiki jana na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Ihefu, leo Jumatano kikosi cha Tanzania Prisons kimeondoka rasmi jijini Mbeya kuelekea mkoani Rukwa ambapo kitacheza mechi zote za Ligi Kuu zilizobaki

Hatua hiyo inajibu maswali ya wadau na mashabiki wa soka waliokuwa wakihoji makao makuu ya klabu hiyo kwa msimu huu baada ya kwuapo kwa taarifa tofauti ikiwamo ya kukaa Mbeya, Dodoma au Rukwa.

Katika msimu uliopita timu hiyo iliweka kambi yake mkoani Rukwa na kucheza mechi zake huko kwenye uwanja wa Nelson Mandela ambapo matokeo yake hayakuwa mabaya kwa kumaliza nafasi ya saba kwa alama 42.

Hata hivyo timu hiyo kwa muda wote wa maandalizi na mechi mbili ilizocheza na kuambulia pointi moja, ilikuwa jijini Mbeya katika ‘camp’ ya Magereza na leo Oktoba 13 imetangaza kuhamia rasmi huko wilayani Sumbawanga.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Jackson Mwafulango amethibitisha kikosi hicho kuondoka leo na kwamba huko ndio itakuwa kambi rasmi ya timu kwa michezo yote iliyobaki.

“Tunaondoka leo na rasmi Rukwa ndio itakuwa kambi yetu kwa msimu mzima nikimaanisha mazoezi na mechi zote za nyumbani, tunaamini hakuna kitakachoharibika” amesema Mwafulango.

Advertisement
Advertisement