Moallin sasa anawasikilizia mabosi wake

Moallin sasa anawasikilizia mabosi wake

KAIMU Kocha Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin amesema kwa sasa hakifirii kupewa timu hiyo moja kwa moja bali anataka kuijenga iwe ya ushindani na kuondoka eneo la kati katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Moallin alisema suala la kupewa timu linahusu uamuzi ya viongozi wake, lakini akili yake kwa sasa ni kuifanya Azam kuwa tishio na kuheshimika na kama itatokea kapewa hatakuwa na hiyana.

“Ni maswali ambayo wengi wamekuwa wakiniuliza kila mara, lakini itoshe kusema kuwa naridhika na hii nafasi niliyopewa,” alisema Moallin na kuongeza;

“Naamini sana katika vijana na kwa muda niliokuwa hapa nitaendelea kuwatumia kwa sababu msingi mzuri unaanzia kwao, hivyo ni matumaini yangu kwa vipaji walivyokuwa navyo tutafikia malengo ya klabu.”

Akizungumzia mchezo wao wa kesho dhidi ya Mbeya Kwanza, Moallin alisema wanaenda kwa tahadhari na kwa kuwaheshimu wapinzani wao.

“Ni mechi tunayotakiwa kurejea hali ya kujiamini kwa wachezaji wangu baada ya kupoteza mchezo wetu wa fainali ya Mapinduzi dhidi ya Simba, hivyo tumejipanga vizuri kwa kuwa sina aliyeko majeruhi,” alisema Moallin.

Azam inaenda kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya saba na pointi 15, wakati Mbeya Kwanza ipo nafasi ya 10 na pointi 11(kabla ya mechi za jana) na hii ni mara yao ya kwanza kukutana katika Ligi Kuu Bara, Mbeya Kwanza ikiwa imepanda msimu huu.