Mkongo amtaka Manji Yanga

Muktasari:
Pia, Zahera ameshtushwa na uwepo wa wachezaji watatu wa Yanga, ambao ndio mara yake ya kwanza kuwaona lakini, akapigwa butwaa kusikia hawapo kwenye orodha ya wachezaji wa mechi za kimataifa zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
ACHANA kabisa na matokeo ya mchezo wa jana usiku ambayo Yanga imeyapata dhidi ya USM Algers pale Algeria, ishu ni kocha wao mpya Mwinyi Zahera. Mkongo huyo ametoa kauli ya kushtusha baada ya kutajiwa jina la bilionea Yusuf Manji na fasta akatamka kauli ambayo inaweza kuzusha gumzo.
Pia, Zahera ameshtushwa na uwepo wa wachezaji watatu wa Yanga, ambao ndio mara yake ya kwanza kuwaona lakini, akapigwa butwaa kusikia hawapo kwenye orodha ya wachezaji wa mechi za kimataifa zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Akizungumza na Mwanaspoti Zahera alisema amemuona straika Matteo Anthony na kubaini ana kipaji cha juu, pia akasema winga kinda Burhan Akilimali na Maka Edward sio wa mchezo mchezo kabisa na wanaweza kuibeba Yanga.
Amesema kama Matteo atakuwa ‘siriaz’ ni kipaji chake hatadumu Yanga kwa muda mrefu na kuelezea kuwa, shida yake kubwa ni kutojituma na kumtaka ajirekebishe.
Pia, ametamka kuwa makinda Akilimali na Maka atawasuka ili kuwa bora kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao huku akishangaa kuelezwa kuwa, hawapo katika orodha ya wachezaji wanaocheza mechi za Kombe la Shirikisho Afrika.
“Yule Matteo ni straika mzuri ni wachezaji wachache hata wa Ulaya wenye ubora wake, tatizo lake nasikia hajitumi sasa, nataka aanze maisha mapya akijituma ili awe bora zaidi,” alisema Zahera.
“Wale wengine wawili (Akilimali na Maka) nao ni wazuri sana na nimeelezwa hawapo katika orodha ya wachezaji wanaoweza kutumika katika mechi za Caf, hilo limenishtua sana ila tutaangalia namna bora ya kufanya.”
Wachezaji wamchongea Manji
Mwanaspoti linafahamu kuwa, wachezaji wa Yanga walikutana na mabosi wao kabla ya kupanda ndege kwenda Algeria na moja ya mambo yaliyozuka ni kutaka kujua hatima ya madai mbalimbali wanayoidai klabu, pia wakafichua kwa Zahera kuhusiana na habari njema za Manji.
Mastaa hao walimweleza Mkongo huyo kwamba, wakati wa Manji walikuwa wakiishi kama Ulaya, lakini tangu ameachia ngazi mambo yamekuwa tofauti.
“Wachezaji wana malalamiko mengi na nimezungumza na mtendaji mkuu kumwambia azungumze nao, lakini vijana wanamtaka mtu anaitwa Yusuf ambaye walifanya kazi naye vizuri sana,” alisema Zahera.
“Nimewauliza huyo Yusuf kwa sasa yuko hapa Tanzania? Wamenijibu yupo hivyo nikirudi Algeria nitamtafuta nizungumze naye, nataka kufanya kazi na wachezaji asubuhi na jioni lakini ni lazima wawe na furaha, nikifanya kazi hapa mashabiki watafurahi.”