Lwandamina awachimba biti Simba

KOCHA mpya wa Azam, George Lwandamina anayekwenda kuchukua mikoba ya Mromania Aristica Cioaba pale Azam FC ametua na biti kali. Lwandamina aliwahi kufanya kazi Yanga miaka ya nyuma na kuwaachia taji moja la ligi na pia akiwapeleka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho hatua ambayo iliwafanya mashabiki wa Yanga kumpokea kwa furaha na kumshangilia ingawa alikuwa anatua timu pinzani.
Lwandamina aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja Azam wenye kipengele cha kuongeza alisema anajua amekuja katika klabu ambayo ushindani mkubwa utakuwa dhidi ya timu mbili kubwa Simba na Yanga katika kutimiza malengo atakayopewa na waajiri wake.
Kocha huyo raia wa Zambia alisema hana wasiwasi na presha hiyo na kwamba yupo tayari kupambana kuirudishia ushindani Azam FC ambayo tayari ameshaisoma na anajua aanzie wapi kazi yake. Alisema Azam haina kikosi kibaya. “Hapa Tanzania mimi sio mgeni tena najua ligi ya hapa na ushindani,najua Azam watataka ubingwa na vita hiyo nitashindana na klabu nyingi lakini kubwa itakuwa ni dhidi ya Simba na Yanga,”alisema Lwandamina.
“Nilikuwa naiangalia Azam walianza vyema ligi lakini baadaye hari ikapungua na kuanza kuanguka ndio nafasi mimi nipo hapa kazi yangu kubwa itakuwa kurekebisha hilo na tuirudishe timu katika mstari.”
BY KHATIMU NAHEKA